IQNA

Utamaduni wa Qur'ani

Mwana kaligrafia wa Libya avuka changamoto kuandika Qur’ani kwa mkono

17:24 - April 05, 2025
Habari ID: 3480498
IQNA-Mkaligrafia wa Libya, Al-Sharif Al-Zanati, amefanikisha ndoto yake ya maisha ya kuandika Qur'ani Tukufu kwa mkono, licha ya changamoto za kibinafsi na kitaaluma.

Safari yake ilianza utotoni alipotambuliwa na mwalimu wake, ambaye pia alikuwa binamu wa baba yake, kuwa ana kipaji cha maandishi mazuri.

Alilelewa katika familia iliyothamini sanaa, na alifundishwa na wakaligrafia mbalimbali, akiwemo Ibrahim Al-Zanati na Mahfouz Al-Buaishi. Mchango mkubwa pia ulitoka kwa Sheikh Abu Bakr Sassi, mkaligrafia wa Mushaf wa Libya wa mwaka 1982, aliyempa moyo kuwa siku moja atakuwa mkaligrafia wa Qur’ani.

Licha ya machafuko ya kisiasa nchini Libya, Al-Zanati aliwasilisha ombi kwa Mamlaka ya Waqfu ya Libya mnamo Machi 2017. Baada ya kukubaliwa, kamati ya usimamizi iliundwa na vibali vya uchapishaji na usambazaji kutolewa. Al-Zanati alitumia kalamu maalum na vifaa sahihi ili kuhakikisha ubora wa kazi. Mwanawe Mohammed alisaidia sana upande wa kiteknolojia, hasa kazi ilipoingia hatua ya kidijitali.

Katika kipindi hicho, Al-Zanati alikuwa akimlea baba yake aliyekuwa na saratani huku akiendelea na mradi. Muda mfupi baadaye, janga la COVID-19 lilizidisha hali kuwa ngumu zaidi, mkewe akaugua, naye akaendelea kuhudumia familia huku akiandika Qur’ani.

Pigo kubwa lilikuja kazini, alipopoteza ajira yake katika idara ya forodha licha ya kuwa na makubaliano ya awali ya kujitolea kwa mradi wa Qur’ani. Alisema hakuwa na tamaa ya sifa binafsi, bali aliongozwa na dhamira ya kuboresha kaligrafia ya Qur’ani.

Kwa mujibu wake, kazi hiyo imesaidia kujaza pengo muhimu katika upatikanaji wa Mushaf wa ndani unaotumika katika vituo vya kuhifadhisha Qur'ani nchini Libya.

3492567

Habari zinazohusiana
captcha