IQNA

Maelfu waandamana Morocco kuunga mkono Gaza, kulaani jinai za Israel 

18:53 - April 14, 2025
Habari ID: 3480541
IQNA – Maelfu ya Wamoroko walikusanyika Jumapili katika mji mkuu, Rabat, kuonyesha mshikamano wao na watu wa Palestina na kulaani uhalifu unaoendelea wa utawala katili wa Israel katika Ukanda wa Gaza. 

Maandamano makubwa yalianza katika Uwanja wa Bab al-Ahad na kuendelea kuelekea jengo la Bunge la Morocco. Licha ya mvua kubwa, umati mkubwa ulitoa kauli mbiu za kuunga mkono Gaza, wakipeperusha bendera za Palestina na kulaani mauaji ya kimbari dhidi ya raia katika eneo la Palestina lililozingirwa kinyama. 

Maandamano hayo yalivutia watu kutoka kote Morocco, wakiwemo wanaume, wanawake, na watoto, pamoja na viongozi wa kisiasa na wa jamii ya kiraia. Waandamanaji watoa nara na kauli mbiu kama  “Salamu kwa Gaza, Salamu kwa Muqawama” (Mapambano ya Kiislamu) na “Maandamano yataendelea hadi Uhusiano na Israel Utakapovunjwa.” 

Maandamano hayo yalijumuisha matukio yanayoonyesha mateso ya raia wa Gaza, na waandamanaji walichoma bendera za Israel kama ishara ya kupinga utawala huo katili. 

Waandaaji walisema maandamano hayo yalilenga kutoa ujumbe kadhaa muhimu: kupinga mauaji ya kimbari Gaza, kuendelea kwa msaada wa wananchi kwa Palestina, kutoka ufalme wa Morocco na nchi zingine zikate uhusiano na utawala haramu wa Israel, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na taasisi za kibinadamu kuchukua hatua za haraka. 

Tangu katikati ya Machi, Gaza imekuwa ikishuhudia ongezeko la operesheni za kijeshi za Israel. Usitishaji wa mapigano dhaifu, ambao ulikuwa umedumu kwa karibu miezi miwili, ulivunjika tarehe 18 Machi wakati Israel ilianza tena mashambulizi yake. Tangu wakati huo, mashambulizi makali ya anga yamekuwa yakilenga sehemu mbalimbali za Gaza, na kuzidi kudhoofisha miundombinu na kuathiri mfumo mdogo wa huduma za afya katika eneo hilo. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, zaidi ya Wapalestina wasiiopungua 51,000 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 110,0000 wamejeruhiwa tangu Israel inazishe  vita vya mauaji ya kimbari Gaza tarehe 7 Oktoba, 2023. Idadi kubwa ya wahanga ni wanawake na watoto. Aidha, zaidi ya watu 11,000 bado hawajulikani walipo, wengi wakihofiwa kufunikwa na vifusi. 

Morocco ni mojawapo ya mataifa kadhaa ya Kiarabu ambayo yalianzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Israel kama sehemu ya Makubaliano ya Abraham ya mwaka 2020. Hata hivyo, wananchi waliowengi wanapinga mapatano hayo na ni waungaji mkono wa harakati za ukombozi wa Palestina.

3492677

captcha