IQNA

Msahafu ulioandikwa kwa mkono India kukabidhiwa Jumba la Makumbusho la Madina

15:22 - July 22, 2025
Habari ID: 3480980
IQNA – Msahafu au nakala adimu ya Qur’an Tukufu iliyoandikwa kwa mkono juu ya kitambaa inatazamiwa kutolewa rasmi kama zawadi kutoka India kwa Saudi Arabia, kwa ajili ya kuonyeshwa katika Jumba la Makumbusho la Qur’an lililo karibu na Msikiti wa Mtume, Al Masjid an Nabawi (SAW) huko Madina.

Mus’haf huu wa kipekee wenye juzuu tano, uliyoandikwa kwa muda wa miaka sita na dada wawili kutoka Bengaluru amabo ni Suraiyya Quraishi na Bibi Tabassum, unapendekezwa kuwa zawadi rasmi ya serikali ya India kwa Ufalme wa Saudi Arabia, kwa mujibu wa taarifa ya tovuti ya Only Kashmir News.

Nakala hiyo imeandikwa kwa mkono kikamilifu juu ya kitambaa kilichoandaliwa maalum, na ilizinduliwa rasmi katika hafla iliyofanyika kwenye Dargah ya Khwaja Moinuddin Chishty huko Ajmer Sharif.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na mamia ya wageni waliokusanyika kushuhudia mus’haf huo na kushiriki katika dua na ibada. Hafla hiyo ilifanyika chini ya uongozi wa Haji Syed Salman Chishty, Mwenyekiti wa Taasisi ya Chishty Foundation, pamoja na masheikh na walezi wa kiroho wa eneo hilo.

Kazi hiyo ya kaligrafia ina kurasa 604, na ilikamilishwa kwa juhudi binafsi za kiroho na wasanii hao wawili wa Kiislamu kutoka India.

Haji Syed Salman Chishty alitangaza nia yake ya kuwasilisha pendekezo rasmi la kutoa mus’haf huo kama zawadi ya kidiplomasia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu wa India.

Katika tamko lake alisema: “Nakala hii tukufu… siyo tu kazi ya ibada, bali ni daraja la kiroho baina ya mataifa yetu.” Alieleza kuwa mahali panapokusudiwa kwa ajili ya mus’haf huu ni Al-Maktabah al-Qur’aniyyah mjini Madina.

Mashauriano na taasisi husika za serikali yanatarajiwa kuanza hivi karibuni ili kurahisisha utekelezaji wa pendekezo hili, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

3493930

captcha