IQNA

Mikakati yawekwa kuhudumia Wafanyaziara wa kike katika Haram ya Najaf wakati wa Arbaeen

7:55 - August 02, 2025
Habari ID: 3481032
IQNA – Idara ya Masuala ya Wanawake ya Taasisi ya Haram Tukufu ya Imam Ali (AS) imeandaa mipango kabambe ya kuwahudumia wafanyaziyara wa kike katika msimu huu wa ziara ya Arbaeen.

Kwa mujibu wa taarifa, idara hiyo imehamasisha watumishi wake wote na kuandaa mpango wa kiusalama na kihuduma kwa ajili ya kuwapokea mamilioni ya wafanyaziyara wa kike watakaoshiriki katika matembezi ya Arbaeen.

Bi Ramla al-Khuzai, mkuu wa Idara ya Masuala ya Wanawake, alisema kuwa mpango mpya wa huduma umeandaliwa katika haram hiyo tukufu. Miongoni mwa mambo muhimu ni kuongeza idadi ya milango ya kuingilia na kutoka ili kupunguza msongamano, na kuweka mfumo maalum kwa wazee ili waweze kufika kwa urahisi moja kwa moja hadi katika haram.

Aliongeza kuwa maeneo maalum yamepangiwa kwa ajili ya wafanyaziyara wa kike, na kuna wafanyakazi na wasimamizi wanaozungumza lugha mbalimbali, kama vile Kifarsi, Kiingereza, na nyinginezo, ili kuhakikisha mawasiliano mazuri na mazingira ya utulivu kwa wafanyaziyara hao.

Kuhusu maendeleo yaliyofikiwa, alieleza kuwa ushirikiano umefanyika na idara husika, mabango yenye maelekezo yamewekwa wazi, na ramani za kuongoza wafanyaziyara ndani ya haram zimeandaliwa.

Vilevile, mfumo wa kisasa wa kuhifadhi na kurudisha vitu vya thamani umeanzishwa kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa wafanyaziyara wa kike, alisema al-Khuzai.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo rasmi, vikosi vya usalama na huduma vimepewa vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya kuwasiliana kwa haraka na kuchukua hatua za dharura, huku timu ya msaada ikifanya kazi saa 24 kushughulikia dharura yoyote.

Aliongeza kuwa idara hiyo itaendelea na jitihada za hali ya juu kuhakikisha wafanyaziyara wa kike wa Arbaeen wanahudumiwa kwa namna bora wanapotembelea haram ya Imam Ali (AS) kabla ya kuelekea Karbala.

Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa na Waislamu wa Kishia siku ya arobaini baada ya Ashura, kuenzi kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam wa tatu wa Kishia.

Ni moja ya ziara kubwa zaidi duniani kila mwaka, ambapo mamilioni ya Waislamu wa Kishia , pamoja na baadhi ya Masunni na wafuasi wa dini nyingine,  hujiunga katika matembezi ya kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen itasadifiana na tarehe 14 Agosti.

4297552

captcha