IQNA

Qari wa Misri atoa wito wa Umoja Miongoni mwa wahudumu wa Qur’ani Tukufu

16:45 - November 02, 2025
Habari ID: 3481451
IQNA – Qari maarufu wa Misri, Abdul Fattah Tarouti, ametoa wito wa kuepuka mifarakano miongoni mwa wahudumu wa Qur’ani Tukufu kufuatia mjadala ulioibuka kuhusu usomaji wa Qari mwenzake, Ahmed Ahmed Nuaina.

Tarouti, ambaye ni Naibu Sheikh al-Qurra (Mkuu wa Wasomaji) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wasomaji wa Qur'ani Misri, alitoa tamko kuhusu maudhui yaliyochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa umoja huo na maoni kuhusu makosa yaliyotokea katika usomaji wa Qur’ani uliofanywa na Sheikh Nuaina.

Alieleza kuwa baada ya maudhui hayo kuchapishwa na Rais wa Umoja huo, Sheikh Muhammad Saleh Hashad, “nilimwasiliana naye na akanifafanulia kuwa usomaji huo ulitangazwa moja kwa moja kutoka Msikiti wa Al-Marsi Abu al-Abbas huko Alexandria kupitia mitandao ya kijamii, na alipewa video hiyo na baadhi ya watumiaji waliomtaka kutoa maoni na ufafanuzi kuhusu makosa yoyote ya bahati mbaya au kusahau katika usomaji wa aya.”

Tarouti aliongeza, “Makosa ya usomaji ni jambo ambalo hakuna mtu asiyeweza kukosea, kwani watu wote wa Qur’ani, wadogo kwa wakubwa, wanakumbwa nalo. Lakini Qur’ani Tukufu ni yenye kushinda na haiwezi kushindwa.”

Aliendelea kusema, “Kiongozi wa umoja alieleza kuwa ametekeleza wajibu wake kwa sababu moja ya malengo makuu ya umoja ni kuhifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu dhidi ya makosa, sambamba na kulinda hadhi na heshima ya msomaji; hakuna anayepaswa kutengwa.”

Tarouti alisisitiza kuwa anamheshimu sana Qari huyo mashuhuri, Dkt. Ahmed Nuaina – binafsi na kama Sheikh al-Qurra wa Misri. “Yeye ni mtu wa thamani kubwa na mwenye hadhi ya juu ambaye hawezi kudhalilishwa wala kuumizwa.”

Tarouti aliendelea kusema kuwa kilichotokea hakina athari kwa mizizi ya mapenzi na heshima inayowaunganisha wanaharakati wote wa Qur’ani. “Hizi ni uhusiano ulioleta nyoyo zetu pamoja kwa mapenzi ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kutekeleza jukumu tukufu la Qur’ani kwa roho safi, nia ya dhati na uvumilivu.”

Alisisitiza kuwa mapenzi na upendo kati ya watu wa Qur’ani ndiyo msingi na roho ya Uislamu.

Tarouti alihitimisha kwa kutoa wito kwa kila mmoja kuepuka kusababisha mifarakano miongoni mwa watu wa Qur’ani, akisema kuwa “lengo letu sote ni kuitumikia Qur’ani na watu wake.”

Hivi karibuni, video ya usomaji wa Ahmed Nuaina ilichapishwa ikionyesha makosa mawili aliyoyafanya. Baada ya video hiyo kutumwa kwa Sheikh Hashad, alitoa tamko rasmi kwenye ukurasa wa umoja huo pamoja na video, akisisitiza kuwa baraza la umoja litafanya kikao hivi karibuni ili kutoa uamuzi mwafaka kuhusu tukio hilo.

Wakati huohuo, Sheikh Nuaina mwenyewe amekataa kutoa maoni kuhusu suala hilo ili kulinda heshima ya maqari wa Misri.

3495228

Habari zinazohusiana
Kishikizo: tarouti qari
captcha