IQNA

Chuo Kikuu cha Qur’ani Tukufu kuanzishwa Pahang, Malaysia

8:18 - February 07, 2026
Habari ID: 3481897
IQNA-Malaysia iko mbioni kuanzisha chuo kikuu maalumu kwa elimu za Qur’ani, kufuatia ridhaa ya Sultan wa Pahang ya kubadilisha jina la taasisi ya elimu iliyopo tayari.

Al-Sultan Abdullah Ri’ayatuddin Al-Mustafa Billah Shah ameridhia kubadilishwa kwa jina la Universiti Islam Pahang Sultan Ahmad Shah (UnIPSAS) kuwa Universiti Al-Quran, hatua itakayokifanya kuwa chuo kikuu cha kwanza cha aina yake nchini humo.

Al-Sultan Abdullah amesema juhudi za kuimarisha na kuinua Uislamu katika jimbo la Pahang zitaimarishwa zaidi kupitia chuo kikuu kitakachojikita katika masomo ya Qur’ani.

Alibainisha kuwa mabadiliko hayo si ya jina pekee, bali ni mwelekeo wazi wa kimkakati unaolenga kuiweka Qur’ani Tukufu kuwa nguzo kuu ya maendeleo ya kielimu na kiroho ya jimbo hilo.

“Uwekaji wa chapa hii ni sawa na kuinua alama muhimu katika jimbo, inayoashiria kwa uwazi mwelekeo na dhamira yake,” alisema katika chapisho kwenye ukurasa rasmi wa Facebook wa Kesultanan Pahang siku ya Ijumaa.

Sultan alikuwa akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mashindano ya 69 ya Qur’ani na Hifdh ya jimbo la Pahang, yaliyofanyika katika Dewan Jubli Perak Sultan Haji Ahmad Shah siku ya Alhamisi.

Al-Sultan Abdullah pia alieleza matumaini yake kuwa chuo kipya cha Universiti Al-Quran, kitakachotangazwa rasmi hivi karibuni, kitaeneza uelewa mpana wa Qur’ani Tukufu na kuzalisha wanazuoni, wahubiri na viongozi watakaoongozwa na wahyi wa Mwenyezi Mungu.

Kabla ya kuwadia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, aliwasihi wananchi kujiandaa kwa ikhlasi na unyenyekevu, akitaja Ramadhani kuwa ni chuo cha kuilea roho na fursa ya kuimarisha uhusiano kati ya mja na Muumba wake.

Habari inayohusiana:

  • Serikali ya Malaysia Kuongeza Fedha kwa Ajili ya Tafsiri za Qur’ani za Taasisi ya Restu

Sultan alisisitiza kuwa uzuri wa Ramadhani unadhihirika katika heshima, uvumilivu na kusaidiana na wenye uhitaji, ili baraka zake ziwafikie wote bila ubaguzi.

Katika hafla hiyo, Zul-Hasyimi Mohamed Yunus alitangazwa mshindi wa kwanza katika kitengo cha Qari, huku Nurul Saadah Mohamad Zaini akishinda katika kitengo cha Qariah.

Chanzo: malaymail.com

3496316

Habari zinazohusiana
captcha