IQNA

Wahitimu wa Vikao vya Qur’ani nchini Yemen waenziwa

15:11 - February 15, 2026
Habari ID: 3481939
IQNA – Hafla maalumu ilifanyika nchini Yemen kuwaenzi wanafunzi 200 waliokamilisha masomo yao katika vikao vya Qur’ani vilivyoendeshwa misikitini katika kitongoji cha Madhbah, Wilaya ya Maeen.

Hafla hiyo iliandaliwa na Idara ya Utamaduni wa Kijihadi, kwa ushirikiano na Ofisi ya Uhamasishaji wa Umma katika Wilaya ya Maeen. Katika hotuba yake, Afisa wa Uhamasishaji wa Umma wa Madhbah Kusini, Ali Al‑Waisi, aliwapongeza walimu na wasimamizi wa vikao vya mawaidha na dhikri kwa juhudi zao katika kufundisha Qur'ani Tukufu na kulea kizazi chenye ufahamu, busara na mwamko wa kiimani, huku wakikiimarisha utambulisho wa Kiislamu na utamaduni wa Qur’ani.

Al‑Waisi alisisitiza kuwa kundi hili la wahitimu ni tunda la kweli la uangalizi na msisitizo mkubwa uliotolewa na kiongozi wa mapinduzi, Abdul‑Malik Badreddin Al‑Houthi, katika kujenga kizazi cha Qur’ani kilicho imara kwa elimu na maadili mema.

Akizungumza zaidi, Al‑Waisi alisema kuwa wanafunzi wa vikao vya Qur’ani ni kielelezo cha juu cha maadili na ubora wa kibinadamu, na akawahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule na vikao vya Qur’ani ili kuwalinda dhidi ya hatari za vita laini (soft war) na njama za maadui zinazolenga vijana na kujaribu kupotosha utambulisho wao wa kiimani.

Vilevile, aliwahimiza wananchi wote kujiandaa kiroho kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuimarisha uhusiano wao na Qur’ani Tukufu, kutafakari aya zake, na kufuatilia kwa makini mihadhara ya Ramadhani ya kiongozi, ambayo huchangia utakaso wa nafsi na kuimarisha utamaduni wa Qur’ani na imani.

Habari inayohusiana:

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Polisi wa Madhbah, Luteni Kanali Muhammad Rajeh, pamoja na masheikh, viongozi wa jamii, wakuu wa mitaa na umati mkubwa wa wakazi. Ratiba ya hafla ilijumuisha hotuba za wahitimu, qiraa na qasida, pamoja na maonyesho mbalimbali ya wanafunzi, yote yakionyesha fahari ya kushikamana na manhaj ya Qur’ani.

Mwisho wa hafla, vyeti vya heshima na zawadi za ishara viligawiwa kwa wanafunzi waliokamilisha masomo yao katika vikao vya Qur’ani.

3496416

Habari zinazohusiana
captcha