IQNA

Msomi wa Nigeria asema, "Hifadhi Qur’ani ili kuinua hadhi ya kidunia na kiroho"

14:22 - April 22, 2026
Habari ID: 3482159
IQNA – Sheikh Hayatu Umar, mhadhiri wa masomo ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Dutsin‑Ma (FUDMA) kilichopo Jimbo la Katsina nchini Nigeria, amewataka vijana na wanafunzi waweke kipaumbele katika kuhifadhi Qur’ani Tukufu, akisisitiza kuwa kufanya hivyo huminua mtu hadhi yake duniani na Akhera.

Aliyasema hayo Jumatatu mjini Dutsin‑Ma, katika hafla ya uzinduzi wa kundi la kwanza la wanafunzi wa Chuo cha Qur’ani na Qirā’at.

Chuo hicho kimeanzishwa mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi Qur’ani kupitia njia mbalimbali za usomaji zinazofuatilia misururu ya mapokezi hadi kwa Mtume Muhammad (SAW).

Akinukuu kauli ya msomi mmoja maarufu, alisema: “Hadhi ya mtu haipandi isipokuwa kwa kile alichokihifadhi na kukijua katika Qur’ani Tukufu.”

Mhadhiri huyo alieleza kuwa watu wa Qur’ani ni waheshimiwa na watu wema zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa wanadamu.

Sheikh Umar, ambaye pia ni mmoja wa walimu wa chuo hicho, alinukuu tena hadith ya Mtume Muhammad (SAW) isemayo: “Bora wenu ni yule ajifunzaye Qur’ani na akawafundisha wengine.”

Alisema njia zote 10 mashuhuri za Qirā’at zinapata thawabu sawasawa, na mtu anaruhusiwa kuchagua mojawapo kwa ajili ya kusoma Qur’ani.

Naye msajili wa chuo hicho, Suleiman Abdullahi, alisema: “Kitengo hiki hupokea wanafunzi waliokwishahifadhi sehemu ya tatu ya Qur’ani, na wanakamilisha Qur’ani nzima ndani ya mwaka mmoja.

“Kuna pia kozi ya cheti ya miezi sita na diploma ya miaka miwili, vyote hivyo kwa wale ambao tayari wameshahifadhi Qur’ani Tukufu.”

Mwenyekiti wa chuo na pia Mkuu wa Wilaya ya Dutsin‑Ma, Kabir Abdussalam‑Shema, pamoja na Sada Muhammad‑Sada, katika salamu zao za pongezi, waliwahakikishia viongozi wa taasisi hiyo kuwa wataendelea kuiunga mkono katika kutimiza malengo yake.

3497171

Kishikizo: qurani tukufu nigeria
captcha