IQNA

Madarasa ya Qur’ani nchini Bosnia yaadhimisha mwisho wa mwaka wa masomo

17:43 - June 10, 2026
Habari ID: 3482347
IQNA – Hafla ya kuadhimisha kuhitimishwa kwa mwaka wa masomo 2025–2026 kwa madarasa ya Qur’ani (Kutab) imefanyika katika mji wa Zenica nchini Bosnia na Herzegovina.

Kwa mujibu wa tovuti ya Muslims Around the World, hafla hiyo iliandaliwa katika ukumbi wa michezo wa Zenica, chini ya usimamizi wa Baraza la Mashikat ya Kiislamu la mji huo.

Tukio hilo, linalodhihirisha nafasi ya elimu ya dini ndani ya jamii ya Waislamu wa Bosnia na Herzegovina, lilishuhudia ushiriki wa takribani wanafunzi 500 wa kike na wa kiume kutoka ngazi ya tatu ya elimu ya Qur’ani. Kadhalika, walimu 79 waliokuwa wakisimamia mafunzo yao walihudhuria hafla hiyo.

Katika hotuba yake kwenye programu hiyo, Anis Safraka, Mkurugenzi wa Idara ya Qur’ani na Vijana ya baraza hilo, alinukuu Hadithi ya Mtume Muhammad (S.A.W.) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alitumwa akiwa mwalimu, na akasisitiza kuwa risala ya Uislamu imejengwa juu ya msingi wa elimu na malezi.

Alieleza kuwa jukumu la mwalimu haliishii katika kufikisha maarifa pekee, bali pia linajumuisha kujenga maadili na tunu, pamoja na kulea vizazi vinavyoweza kuitumikia jamii yao.

Safraka alisema walimu wanabeba dhamana kubwa ya kuimarisha hekima na fadhila katika taasisi za elimu, na kuwasaidia vijana kuelewa misingi ya Kiislamu na kuitekeleza katika maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Mufti wa Zenica, Mlodin Dizdarovic, katika hotuba yake alisisitiza kuwa shule za elimu ya Qur’ani ni miongoni mwa vituo muhimu zaidi vya kuhifadhi utambulisho wa kidini, kimaadili na kitamaduni wa jamii ya Waislamu nchini humo.

Alisema kupitia shule hizi, watoto hupata tunu na misingi itakayobaki nao katika maisha yao yote, na kuwaongoza kuelekea kwenye uwajibikaji na kuitumikia jamii.

Hafla hiyo pia ilijumuisha utoaji wa tuzo kwa idadi ya wanafunzi waliobobea, kupitia tuzo ya “Heshima ya Kutab”, ambapo mwanafunzi mmoja kutoka kila msikiti au kituo cha elimu alichaguliwa kwa kuzingatia juhudi zake, kujituma kwake, ubora wake katika masomo, na mwenendo mwema.

Waandaaji walisema kuwa zaidi ya wanafunzi 6,000, pamoja na walimu 79, hushiriki mara kwa mara katika programu za madarasa ya Qur’ani ya Zenica, jambo linaloonesha nafasi muhimu ya mfumo huu wa elimu katika maisha ya jamii ya Waislamu.

Pia walibainisha kuwa shule ya Qur’ani si darasa la kufundisha Qur’ani Tukufu pekee, bali ni taasisi kamili ya malezi na elimu yenye mchango mkubwa katika kuandaa vizazi vyenye maadili, uwajibikaji, na ufahamu wa dini.

Zenica ni miongoni mwa miji mikubwa zaidi nchini Bosnia na Herzegovina, ulioko katikati ya nchi hiyo. Mji huu una jamii hai ya Waislamu pamoja na idadi kubwa ya taasisi za elimu na dini zilizo chini ya Jumuiya ya Kiislamu ya Bosnia na Herzegovina ambazo huzingatia malezi bora ya vijana

3497778

captcha