IQNA

18:56 - August 20, 2026
Habari ID: 3482651

Kiongozi wa Kikristo Nigeria ampongeza mwanazuoni wa Kiislamu kwa huduma ya miaka 50

IQNA – Kiongozi wa Kikristo katika Jimbo la Kaduna nchini Nigeria amemuenzo mwanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Usman Mohammed Mai-Mota (Gwalli), kwa kutambua mchango wake wa zaidi ya nusu karne katika kutoa elimu ya Kiislamu na kuwafundisha maelfu ya vijana, katika juhudi za kuimarisha kuishi kwa amani na mshikamano kati ya Wakristo na Waislamu.

nigeria

Mchungaji Dkt. Yohanna Buru, Msimamizi Mkuu wa Christ Evangelical and Life Intervention Ministry, aliongoza ujumbe wa viongozi wa Kikristo kwenda katika madrasa ya Sheikh Usman, ambako walimkabidhi tuzo ya kutambua mchango wake katika elimu ya Kiislamu na maendeleo ya jamii.

Mchungaji Buru alisema Sheikh Usman ametumia zaidi ya miaka 50 kuwafundisha watoto na vijana kutoka maeneo mbalimbali ya kaskazini mwa Nigeria Qur’ani, Hadith, Tafsiri, lugha ya Kiarabu na masomo mengine ya Kiislamu.

Alisema wanafunzi wengi wa zamani wa mwanazuoni huyo wameendelea kuwa wanazuoni wa Kiislamu, walimu wa Kiarabu na wahadhiri katika shule, vituo na taasisi mbalimbali nchini humo.

Ujumbe huo ulisema tafiti zilizopo zinaonyesha kuwa Sheikh Usman amewahi kuwafundisha zaidi ya vijana 10,000, ambao wengi wao sasa wanafanya kazi kama walimu wa Kiarabu, wanazuoni wa Kiislamu na wahadhiri katika maeneo mbalimbali ya kaskazini mwa Nigeria.

Mchungaji Buru alisema kutambuliwa kwa mwanazuoni huyo kulilenga si tu kumtia moyo kuendelea na kazi yake ya kielimu licha ya umri wake mkubwa, bali pia kuimarisha uhusiano kati ya Wakristo na Waislamu katika Jimbo la Kaduna.

Mchungaji Emmanuel John, ambaye alikuwa miongoni mwa ujumbe huo, alielezea mchango wa Sheikh Usman kuwa wa kipekee, akisema ziara hiyo ililenga kukuza kuheshimiana, amani na uelewano kati ya jumuiya hizo mbili za kidini.

Sheikh Usman alieleza shukrani zake kwa kutambuliwa huko, akisema hiyo ilikuwa tuzo ya kwanza aliyowahi kupokea katika zaidi ya miaka 50 ya kufundisha. Alisema heshima hiyo imempa ari mpya ya kuendelea kuwaelimisha vijana Waislamu licha ya umri wake mkubwa.

3498680

captcha