IQNA

23:23 - February 15, 2021
Habari ID: 3473653
TEHRAN (IQNA)- Maafisa wa serikali ya Yemen wanasema nchi yao hivi imo vitani, inashambuliwa kila uchao na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia, hivyo ni haki ya kawaida kabisa kwa wananchi wa Yemen kujibu mashambulizi wanayofanyiwa.

Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen ameyasema hayo Jumapili katika mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, wavamizi wa nchi yetu bila ya shaka hadi sasa wameshapata ujumbe kwamba jeshi la Yemen halina hamu ya kumshambulia mtu wala kundi lolote lakini ni haki yake kujihami.

Aidha ameziambia nchi vamizi zinazoongozwa na Saudi Arabia na waungaji mkono wao kwamba badala ya kujitia pamba masikioni na upofu machoni na kujifanya kutoona wala kusikia jinai wanazofanyiwa wananchi wa Yemen, madola hayo yatekeleze majukumu yao na yaache kulilaumu jeshi la nchi hiyo kila linapojibu jinai wanazofanyiwa wananchi wa Yemen.

Katika upande mwingine, Brigedia Jeneli Yahya Sarii, msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen jana Jumapili alitangaza habari ya kushambuliwa uwanja wa ndege wa Abha wa Saudi Arabia na kusema kuwa, maeneo yaliyokusudiwa ndani ya uwanja huo yamelengwa kwa ustadi mkubwa na vikosi vya Yemen ikiwa ni majibu ya jinai zinazofanywa na Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen.

Wakati huo Huo Muhammad Ali Al-Houthi, mwanachama mwandamizi wa Baraza Kuu la Kisiasa Yemen amesema Jeshi la Yemen,  likishirikiana na Kamati za Wananchi , litaendelea kutumia makombora na ngege zisizo na rubani kutekeleza hujuma ndani kabisa ya ardhi ya Saudia na waitifaki wake. Amesema mashambulizi hayo yataendela maadamu Saudia na waitifaki wake wanaendelea kuishambulia Yemen. Ameongeza kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudia ukisitisha hujuma zake, basi Yemen nayo itasitisha mashambulizi.

Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen wakiongozwa na Harakati ya Ansarullah. Harakati hiyo imekuwa ikitekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya ardhi ya Saudi Arabia ambapo imeleng mara kadhaa vituo vya kusafisha mafuta na pia viwanja vya ndege vinavyotumiwa na jeshi vamizi la utawala huo wa kifalme.

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na vita vya Saudia dhidi ya nchi hiyo..

Aidha mwezi Disemba mwaka jana,  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

3473976

Kishikizo: Yemen ، saudia ، ansarullah
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: