IQNA

Saudia yasema Umrah inaruhusiwa tu kwa wenye umri wa miaka 18 hadi 50

19:28 - November 19, 2021
Habari ID: 3474578
TEHRAN (IQNA)- Idhini ya kutekeleza Hija ndogo ya Umrah kwa wale wanaotoka nje ya Saudia itajumuisha tu wale wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 50.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Hija na Umrah ya Saudi Arabia ambayo imeongeza kuwa wanaotekeleza ibada ya Umrah wanapaswa kuwa wamepata chanjo kamili ya COVID-19 na chanjo iliyotumika iwe ni ile ambayo inatambuliwa na Saudia. Aidha wanaoingia nchini humo wanatakiwa kuwa na cheti rasmi cha kuonyesha wamepata chanjo kabla hawajapokea Visa ambayo inatumwa kwa njia ya intaneti kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia.

Halikadhalika wanaotekeleza ibada ya Umrah wametakiwa kutumia mawakala rasmi wa usafiri ambao watawasaidia kupata vibali vyote vya kutekeleza ibada ya Umrah na kuswali katika Msikiti Mtakatifu wa Makka.

Hivi karibuni huduma mpya imezinduliwa kwa ajili ya Waislamu walionje ya Saudi Arabia ambao wanataka kutekeleza Hija ndogo ya Umrah.

Shirika la Habari la Saudia  (SPA) limeandika kuwa: "Kwa ushirikiano na Mamlaka ya Data na Akili za Kubuni au Artificial Intelligence Saudia (SDAIA), Wizara ya Hija na Umrah inatangaza kuzinduliwa huduma mpya ambayo itawawezesha wale walio nje ya nchi kupata  vibali vya Umrah na Sala katika Msikiti Mtakatifu wa Makka na pia kuzuru Msikiti wa Mtume SAW kwa kujisajili kupitia Aplikesheni za 'Eastmarna' na 'Tawakkalna'.

Wizara hiyo imesema aplikesheni hizo zitaweza kutumika punde baada ya wageni wanaoingia nchini humo kujisajili katika tovuti ya "Quddum" ambayo ni maalumu kwa wale wanaowasili Saudia.

Oktoba 16 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia ilitangaza kupunguza vizuizi ambavyo vilikuwa vimewekwa katika ufalme huo ili kuzuia maambukizi wa COVID-19. Kwa mujibu wa kanuni mpya ni ruhusha waumini kujaa kama kawaida katika Msikiti Mtakatifu wa Makka na Msikiti wa Mtume SAW mjini Madina.

3476552/

Kishikizo: hija umrah saudia
captcha