Imam Marcellus “Khaliifah” Williams, Muislamu, alinyongwa Jumanne Septemba 24 jioni kufuaia hukumu ya mahakama.
Majaji wa Mahakama ya Juu Sonia Sotomayor, Elena Kagan na Ketanji Brown Jackson walikuwa na uwezo wa kukubali ombi la kuzuia kunyongwa kwake lakini hawakufanya hivyo.
Katika taarifa yake ya mwisho, Williams aliandika, “Sifa Zote Anastahiki Allah Katika Kila Hali.” Kulingana na Idara ya Marekebisho ya Missouri, mtu wa mwisho kumtembelea alikuwa Imam Jalahii Kacem.
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), shirika kubwa zaidi la kutetea haki za Waislamu wa Marekani, limelaani hatua hiyo.
Zaidi ya watu 60,000 walikuwa wametia saini waraka wa CAIR wa kumtaka Gavana Parson kusitisha utekelezaji wa hukumu hiyo ya kidhulma.
Katika taarifa, Naibu Mkurugenzi wa Kitaifa wa CAIR Edward Ahmed Mitchell alisema:
"Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea. Kwa kumhukumu kifo Imam Marcellus Williams, licha ya kwamba hata mwendesha mashtaka amesema kesi yake iligubikwa na makosa ya kikatiba na kwamba ushahidi wa DNA unaonyesha kutokuwa na hatia, Mahakama ya Juu ya Marekani na mfumo wa mahakama ya Missouri umefanya kosa kubwa dhidi ya ubinadamu".
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Tunalaani vikali unyongaji huu mbaya na usio wa haki, ambao utatia doa sifa ya mfumo wetu wa sheria kwa miaka mingi ijayo. Tunawahimiza Waislamu wote wa Marekani kumuombea dua Imam Williams. Mwenyezi Mungu amlipe kwa kukabiliana na miongo ya dhulma kwa uthabiti, na Mungu amjaalie daraja la juu kabisa la Pepo.”
Williams, Mwislamu mwenye asili ya Afrika aliyekuwa na umri wa miaka 55 ambaye alihudumu kama Imamu wa kitengo chake cha gereza, aliuawa kwa kudungwa sindano ya sumu katika gereza la serikali huko Bonne Terre, Missouri, licha ya ushahidi wa DNA uliomwondolea hatia na makosa ya kikatiba katika kesi yake ya 1998.
Upimaji wa hivi majuzi wa DNA "ulimwondola hatiani" Williams tangu mwaka wa 2017, wakati Gavana wa wakati huo Eric Greitens alipozuia kunyongwa kwake kutokana na vipimo vya DNA vilivyoonyesha DNA ya mtu ambaye hajatambuliwa kwenye silaha ya mauaji.
Licha ya ushahidi huu, na makosa ya wazi ya kikatiba katika kesi yake, Jaji Bruce Hilton alikataa ombi la kufuta hukumu ya Williams na hukumu ya kifo.
3490035