Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya utawala wa Israel, Kombora hilo lilitua katika eneo la Gush Dan jijini Tel Aviv, eneo kubwa zaidi la viunga katika maeneo hayo na kitovu cha sekta ya kifedha na teknolojia ya hali ya juu katika utawala wa Israel, siku ya Alhamisi.
Taarifa zinadokeza kuwa kumejiru uharibifu mkubwa wa magari katika kitongoji cha Ramat Aviv kaskazini magharibi mwa Tel Aviv kufuatia shambulio hilo la Jeshi la Yemen.
Huduma ya ambulensi ya utawala wa Kizayuni, wakati huo huo, iliripoti idadi kubwa majeruhi kati ya wale waliokuwa wanakimbia kujificha kwenye mahandaki katika maeneo mbali mbali..
Msemaji wa Jeshi la Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree alisema atatoa "taarifa muhimu" katika saa zijazo.
Jeshi la Yemen limekuwa likiendesha mamia ya mashambulizi dhidi ya Israel tangu tarehe 7 Oktoba 2023, wakati utawala wa Israel ulipoanza kutekeleza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza chini ya uungaji mkono wa Marekani. Tangu wakati huo hadi sasa Israel imeua Wapalestina zaidi ya 46,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Jeshi la Yemen limesisitiza kuwa litaendelea kuishambulia Israel hadi utawala huo utakapomaliza vita vyake dhidi ya Gaza.
3491111