Msafara huo, uliobeba zaidi ya mashua 50 na wajumbe kutoka mataifa 44, uliondoka Barcelona mwezi uliopita kwa lengo la kupinga kile ambacho mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakikitaja kama moja ya vizuizi vikali zaidi duniani.
Waandaaji walieleza safari hiyo kuwa juhudi kubwa zaidi ya baharini ya aina yake kwa miongo kadhaa. Ripoti zinasema majeshi ya doria ya Israeli yaliingilia kati mashua kadhaa umbali wa maili 90 kutoka Gaza, yakilenga mashua kama Yulara na Meteque kwa kutumia mizinga ya maji.
Katika taarifa ya Alhamisi, Harakati ya Kiislamu ya Kupingania Ukombozi wa Palestina,Hamas, ilieleza shambulizi hilo la majini kuwa “uvamizi wa hila, jinai ya uharamia, na ugaidi wa baharini.”
Harakati hiyo imenaini kuwa, “Tunalaani kwa maneno makali kabisa hujuma ya kinyama iliyozinduliwa na adui dhidi ya Msafara wa Sumud, na tunasisitiza kuwa kuuzuia msafara huo ni kitendo cha jinai kinachopaswa kulaaniwa na watu huru duniani kote.”
Hamas pia ilisifu azma ya wanaharakati waliolenga kuvunja mzingiro wa Israeli dhidi ya Gaza, ikihimiza maandamano ya kimataifa na kulaani hadharani uvamizi huo.
Taarifa ya Iran
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali kitendo cha utawala ghasibu wa Israel cha kuivamia kijeshi msafara wa kimataifa wa meli unaojulikana kama Sumud uliokuwa ukielekea Ukanda wa Ghaza kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu na kuvunja mzingiro Tel Aviv dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Esmail Baqaei leo Alhamisi ametoa taarifa na kueleza kuwa ukatili uliofanywa na Israel unadhihirisha ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kukitaja kitendo hicho kuwa ni ugaidi. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesifu na kupongeza juhudi za kibinadamu za wanaharakati wa Flotilla na makundi mengine madogo kutoka nchi mbalimbali duniani kusema wanaharakati hao "wamesimama kidete na kudhihirisha mshikamano na watu wa Palestina.Boti nyingi za msafara wa kimaataifa wa meli zipatazo 50 unaojulikana kama (Sumud) zilivamiwa jana na jeshi la wanamaji la Israel zilipokuwa zikikaribia katika ukanda wa pwani.
Idadi isiyojulikana ya wanaharakati wa msafara huo wa kimataifa walitiwa mbaroni na mawasiliano ya meli hizo na ulimwengu wa nje yalikatizwa na jeshi la lsrael. Jeshi la Israel limeuvamia kijeshi msafara wa kimataifa wa meli kwa jina la (Sumud) huku utawala huo ukiendeleza mashambulizi na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Kamati ya Kimataifa ya Kuvunja Mzingiro wa Gaza ilitaja shambulizi hilo kuwa “jinai ya kivita.”
Venezuela ilitoa tamko kali, ikisema kuwa “tishio halisi kwa amani ya dunia ni uzayuni, itikadi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi inayokiuka kwa mfumo sheria za kimataifa na utu wa binadamu.”
Nchi ya Uturuki pia ilieleza kuwa Israeli inakiuka “sheria za kimataifa kwa kiwango cha juu kabisa,” na ikataja shambulizi hilo kuwa “kitendo cha kigaidi” dhidi ya raia.
Serikali za Ulaya zimebainisha wasiwasi wao. Ufaransa ilihimiza Israeli kuhakikisha usalama wa washiriki wa msafara, huku Waziri wa Mambo ya Nje Jean-Noel Barrot akisema Paris inatarajia washiriki hao kupewa ulinzi wa kibalozi na njia salama ya kurejea nyumbani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland, Simon Harris, alieleza kuingiliwa kwa msafara huo kuwa “jambo la kutia wasiwasi,” akisisitiza kuwa msafara huo ulikuwa juhudi ya amani kuangazia janga la kibinadamu la Gaza.
Italia na Ugiriki zilituma wito wa pamoja kuhusu usalama wa washiriki, huku Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez akisema wanaharakati hao “hawawakilishi hatari au tishio kwa Israeli” na akaitaka Tel Aviv kutowadhuru.
Nje ya bara Ulaya, kauli zilikuwa kali vilevile. Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alilaani kile alichokiita “shambulizi la kikatili,” akitaka kuachiliwa kwa wanaharakati waliokamatwa. “Jinai yao ilikuwa kubeba msaada kwa watu wa Palestina waliokosa msaada,” aliandika.
Waziri Mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim, alishtumu Israeli kwa kuonyesha “dharau ya hali ya juu si tu kwa haki za Wapalestina bali pia kwa dhamira ya dunia,” akiahidi kufuatilia uwajibikaji kwa njia za kisheria.
Rais wa Colombia, Gustavo Petro, alichukua hatua zaidi kwa kutangaza kufukuza wanadiplomasia wote wa Israel nchini mwake. Alisema kuingiliwa kwa msafara huo ni “jinai mpya” ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na kuthibitisha kuwa raia wawili wa Colombia walikuwa ndani ya msafara huo.
Kadri lawama za kimataifa zinavyozidi kuongezeka, waandaaji wa msafara huo wanasisitiza kuwa dhamira yao ni mshikamano na msaada wa kibinadamu kwa Gaza, ambako zaidi ya watu 66,000 wameuawa tangu Oktoba 2023 kutokana na vita vya mauaji ya halaiki vinavyoendeshwa na Israel.
3494843