IQNA

Msomi: Ni Muhimu kutumia fursa ya Maonyesho ya Qur’ani kutambulisha neno la Wahyi duniani

15:42 - January 14, 2026
Habari ID: 3481800
IQNA – Afisa na msomi mmoja wa masuala ya Qur’ani Tukufu nchini Iran amesisitiza umuhimu wa kutumia uwezo na nafasi ya Maonyesho ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Tehran yanayokuja ili kulitambulisha neno la Wahyi kwa watu wa ulimwengu.

Hujjatul Islam Hamid Reza Arbab Soleimani, mkuu wa Kituo cha Qur’ani na Etrat katika Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu Iran, aliyasema haya katika kikao kilichofanyika Tehran Jumanne kujadili maandalizi ya toleo la 33 la maonyesho hayo.

Akitaja uwepo wa wageni wa kimataifa katika maonyesho hayo, alisema kuna haja ya mipango madhubuti ili kutumia vyema fursa hiyo.

Akasema kuwa kwa msaada wa wanaharakati wa Qur’ani, kutafanyika jitihada za kuitambulisha Qur’ani kwa dunia kwa njia iliyo bora zaidi.

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, afisa huyo aligusia vitendo vya kutusi Qur’ani vilivyotokea katika machafuko ya hivi karibuni nchini Iran, akisema kuwa hatua kama hizo zinatokana na kushindwa kwa wahusika kutambua utamaduni wa juu wa watu wa Iran pamoja na utambulisho wao wa kidini na wenye misingi ya maadili.

Katika kikao hicho, mapendekezo na mawazo mbalimbali yaliwasilishwa kuhusu kuandaa sehemu ya kimataifa ya maonyesho yajayo ya Qur’ani.

Ilibainishwa kuwa sehemu hiyo ya kimataifa, kwa kuzingatia diplomasia ya Qur’ani, itakuwa jukwaa la kuikuza Qur’ani Tukufu kama chombo cha kuleta ukaribu wa kitamaduni, kiroho na kielimu miongoni mwa Ummah wa Kiislamu.

Kutakuwa na majukwaa ya mijadala, mikutano, shughuli za kitamaduni na sanaa, warsha maalumu, pamoja na kuwaheshimu wanaharakati wa kimataifa wa Qur’ani, yote yakiwa na lengo la kuinua diplomasia ya Qur’ani na kuongeza mwingiliano wa kitamaduni na kiakili kati ya mataifa na taasisi za Qur’ani duniani.

Pia kutakuwa na mabanda yatakayoonyesha shughuli za Qur’ani za nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa za Qur’ani, yakitoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kuunda mitandao ya ushirikiano miongoni mwa wanaharakati wa Qur’ani duniani.

Maonyesho ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Tehran hufanyika kila mwaka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa uratibu wa Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu ya Iran.

Kupitia programu mbalimbali kama vikao maalumu, warsha za elimu, makongamano ya Qur’ani, na shughuli mahsusi kwa watoto na vijana, tukio hili la kimataifa linalenga kueneza dhana na shughuli za Qur’ani.

Maonyesho haya pia ni jukwaa la kuonyesha mafanikio mapya ya Qur’ani nchini Iran pamoja na bidhaa mbalimbali zinazolenga kuikuza Qur’ani Tukufu.

3496057

Habari zinazohusiana
captcha