
Akizungumza na IQNA katika maadhimisho ya miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Bilal Al‑Laqis alisema kuwa leo Iran, kwa nguvu yake ya kitamaduni na mtazamo wake wa Qur’ani, imekuwa chanzo cha hamasa kwa mataifa yanayotafuta haki, kwa sababu imefanikiwa kuunganisha dini na maisha ya kila siku pamoja na maendeleo na ustawi.
Bilal Al‑Laqis alizaliwa mwaka 1977 mjini Baalbek, Lebanon. Ana shahada ya uzamivu (PhD) katika sayansi ya siasa na mahusiano ya kimataifa. Anaandika kama mchambuzi kwa vyombo vya habari vya Kiarabu kama Al‑Mayadeen, Al‑Manar, Arabi 21 na Rai Al‑Youm, na pia ni mhadhiri wa chuo kikuu mjini Beirut. Mtazamo wake ni wa kitaaluma na kigeopolitiki kuhusu maendeleo ya kisiasa katika eneo, hususan yanayohusiana na mhimmili wa muqawama (resistance) na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
IQNA: Kama unavyojua, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalijengwa juu ya dhana kama haki, uhuru na heshima ya mwanadamu. Je, inaweza kusemwa kuwa Mapinduzi haya yalikuwa ni kurejea kwenye mafundisho ya asili ya Qur’ani?
Al‑Laqis: Kwa kurejea aya za Qur’ani Tukufu, tunaweza kusema kwamba lengo kuu la Qur’ani yote na hukumu zake ni kuzingatia kwa kina heshima ya mwanadamu, kama Mwenyezi Mungu anavyosema:
“Na hakika tumewahishimu wana wa Adam.”
Hoja kuu hapa ni heshima ya binadamu, kisha mafundisho yote yanayojengwa juu yake. Imam Ali (AS) pia alisisitiza sana juu ya heshima ya mwanadamu.
Jambo jingine muhimu ni kwamba hakuna kitu kinacholingana na thamani na utukufu wa mwanadamu. Kwa hiyo, heshima ya binadamu ndiyo kitovu cha masuala yote, yakiwemo masuala mawili yasiyotenganishwa: haki, ambayo ni tafsiri ya kweli ya heshima, na uhuru, ambao bila huo heshima haiwezi kuwepo.
Aidha, Qur’ani Tukufu ina aya nyingi zinazoonesha kuwa mwanadamu ana uwezo wa kuchagua, jambo linalomtenganisha na viumbe wengine wa Mwenyezi Mungu.
Tunapoangalia pia maisha ya Manabii, tunaona kuwa lengo lao kuu lilikuwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika minyororo ya ndani na ya nje, jambo linalotokana moja kwa moja na heshima ya kibinadamu. Kwa maana hiyo, jamii isiyo na heshima haiwezi kuwa na uhuru wa kweli wa maamuzi.
IQNA: Kwa mujibu wa aya za Qur’ani Tukufu, kupambana na dhulma na uonevu ni miongoni mwa wajibu muhimu zaidi wa Manabii (AS). Je, viongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu waliwezaje kuhamisha mafundisho haya kutoka kwenye eneo la nadharia kwenda kwenye uwanja wa vitendo na mapambano ya kijamii?
Al‑Laqis: Yeyote anayefuatilia hotuba na msimamo wa Imam Khomeini (RA) wakati wa Mapinduzi, na pia misimamo ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Sayyid Ali Khamenei, atagundua wazi kwamba Mapinduzi haya yalitokana moja kwa moja na dhana za msingi za Uislamu, zilizochukuliwa kutoka katika chanzo chake halisi.
Kwa mujibu wa uelewa wetu wa dini ya Mtume Muhammad (SAW), yale yanayotokana na Qur’ani, Manabii na Ahl‑ul‑Bayt (AS) huepuka upungufu, upotovu na dosari.
Sifa ya kipekee ya Imam Khomeini (RA) ilikuwa ni kwamba aliichukua misingi ya Mapinduzi moja kwa moja kutoka Uislamu halisi na safi, bila kuathiriwa na mifumo au falsafa za dini au itikadi nyingine. Pia tunaona katika wasia wake wa kisiasa na kiroho kwamba unaanza na Hadith ya Thaqalayn, ambayo inasisitiza kuwa Qur’ani Tukufu na Ahl‑ul‑Bayt (AS) lazima viambatane pamoja ili kufikia lengo la juu kabisa la mwanadamu.
Kwa msingi huo, inaweza kusemwa kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ni miongoni mwa neema kubwa zaidi katika zama hizi. Miongoni mwa hatua zake muhimu zaidi ni kukataa fikra ya maelewano yasiyo ya haki na dhulma pamoja na mdhalimu, na pia kukataa kuhalalishwa kwa uonevu unaofanywa kwa jina la dini.
Habari inayohusiana:
Kwa sababu katika historia yote hadi leo, kumekuwapo watawala waliowadhulumu watu kwa jina la Uislamu, na dhulma yao ikahalalishwa na baadhi ya wanazuoni wa dini. Hili ni jambo hatari zaidi linalokabili umma wa Kiislamu.
Kwa hiyo, miongoni mwa mafanikio makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba yaliunda njia mpya:
njia ya kuwakabili madhalimu, kuwaangusha watawala wa kiimla, kupanga na kusimama upande wa waliodhulumiwa, na kupambana na dhulma bila kusita.
Licha ya matatizo, vikwazo na gharama kubwa walizokumbana nazo, Jamhuri ya Kiislamu na taifa kubwa na lenye hekima la Iran limeendelea kupambana kwa karibu miaka hamsini, na leo Jamhuri ya Kiislamu imepata nafasi yenye ushawishi mkubwa na athari pana katika dunia.
Hii ina maana kwamba Iran haijawahi kuhalalisha dhulma ya madhalimu kwa namna yoyote ile, na uzoefu huu, pamoja na gharama kubwa iliyolipiwa, ni uzoefu muhimu sana ambao pia umezaa mafanikio makubwa.
3496379