IQNA

Sheikh Naim Qassem: Siku ya Kimataifa ya Quds na nafasi muhimu katika kukombolewa Palestina

11:57 - March 14, 2026
Habari ID: 3482057
IQNA – Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds imechochea uungwaji mkono wa kimataifa kwa kadhia ya Palestina.

Sheikh Naim Qassem alitoa kauli hiyo katika hotuba yake siku ya Ijumaa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds. Katika hotuba yake, Sheikh Qassem alitoa onyo kali kwa Benjamin Netanyahu baada ya waziri mkuu  huyo wa utawala wa kigaidi wa Israel kumtishia kumuua. “Tishio lako la kuniua halina ladha wala thamani yoyote. Wewe ndiye unayepaswa kuogopa kwa ajili ya nafsi yako,” alisema.

Alithibitisha tena azma ya Hizbullah akisema: “Katika kamusi yetu hakuna kitu kinachoitwa kushindwa au kujisalimisha. Tutaendelea kuwa imara katika uwanja wa mapambano bila kujali dhabihu na sadaka zitakazotolewa. Haturudi nyuma, kwa sababu suala hili linahusu uwepo wetu; hii ni vita vya uwepo, si mapambano madogo au rahisi.” ‘Adui atashangazwa katika uwanja wa mapambano’ “Tumejiandaa kwa makabiliano ya muda mrefu. Watashangaa katika uwanja wa mapambano; adui ataona nguvu zetu, na vitisho vyake havitutishi,” Sheikh Qassem alisisitiza.

Alionya kuhusu hatima ya Lebanon bila ya Muqawama a mapambano akisema: “Hakuna suluhisho isipokuwa kupitia muqawama; vinginevyo, Lebanon inaelekea kufutika.” Sheikh Qassem alisisitiza kuwa nchi hiyo inakabiliwa na tishio la uwepo kutokana na mashambulizi ya Israel, akiyataja kuwa “uchokozi hatari na wa kikatili.” Aliongeza: “Hatukuwa katika hali ya kawaida; badala yake tulikuwa tukikabili vitendo vya kinyama ambavyo vimeendelea kwa miezi 15.” Katibu Mkuu wa Hizbullah alikuwa akirejea ukiukaji wa mara kwa mara wa utawala huo dhidi ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwaka 2024 kati ya Tel Aviv na Hizbullah, ambayo yalitarajiwa kumaliza ongezeko la mashambulizi dhidi ya Lebanon. Amesema Hizbullah ilifanya mashauriano katika ngazi za juu za uongozi kupitia mikutano mitatu kabla ya kuamua kukabiliana na uchokozi huo.

Mbali na ukiukaji huo, Hizbullah pia imechochewa kukabiliana na uchokozi kutokana na ushiriki wa hivi karibuni wa utawala huo katika uchokozi wa pamoja na Marekani dhidi ya Iran, uliosababisha kuuawa shahidi kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei pamoja na maovu mengine mengi.

Kiongozi huyo wa Hizbullah pia alizungumzia Siku ya Kimataifa ya Quds, tukio lililowekwa na mwanzilishi marehemu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini, kwa lengo la kuhamasisha uungwaji mkono wa kimataifa kwa harakati za ukombozi wa Palestina dhidi ya ukaliaji na uchokozi wa Israel.

Sheikh Qassem alikumbusha maneno ya Imam Khomeini akisema kuwa Siku ya Quds “ni siku ya kimataifa ambayo haijahusishwa na Quds peke yake, bali ni siku ya waliodhulumiwa kusimama dhidi ya madhalimu.” Aliongeza: “Siku hii ina ishara ya mwito wa kuikomboa Palestina, na pia ina ishara ya kuwafikia wote wanaodhulumiwa duniani ili waachiliwe kutoka katika nira ya utumwa na dhuluma.” Alilaani kuendelea kwa ukaliaji wa Palestina unaoungwa mkono na nchi za Magharibi, akisema kuwa ukaliaji huo “ndio dhuluma kubwa zaidi duniani leo.”

Sheikh Qassem pia aliishutumu Marekani na baadhi ya madola makubwa kwa kudhamini na kuhalalisha ukaliaji huo mwaka 1948, akiuelezea kama “uvimbe wa saratani.” Kama mfano wa uhalifu wa utawala huo unaoungwa mkono na Magharibi, alitaja vita vinavyoendelea vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza ambavyo hadi sasa vimesababisha takriban watu 260,000 kuuawa au kujeruhiwa.

Sheikh Qassem alithibitisha tena uungwaji mkono wa Hizbullah kwa Palestina akisema: “Sisi kama Hizbullah na Muqawama wa Kiislamu tutaendelea kuwa pamoja na Palestina; tunaunga mkono na kuisimamia hadi ukombozi kamili.” Kiongozi huyo wa muqawama alisisitiza wajibu wa pamoja akisema: “Watu wote wa Kiarabu na Kiislamu wana wajibu wa kusimama pamoja na al-Quds na Palestina, kama walivyo na wajibu watu wote huru duniani, kwa sababu kwa kufanya hivyo wanasimama kwa ajili yao wenyewe dhidi ya madhalimu.”

 

3496745

Habari zinazohusiana
captcha