IQNA

Sheikh Qassem: Hizbullah haitasalimu amri mbele ya vitisho

10:39 - February 17, 2026
Habari ID: 3481947
IQNA – Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kuwa harakati hii ya Muqawama au mapambano ya Kiislamu iko tayari kikamilifu kuitetea Lebanon na kamwe haitasalimu amri mbele ya vitisho.

Sheikh Naim Qassem alisema kuwa harakati hii ya Muqawama ya Lebanon haitaki vita, lakini iko tayari kikamilifu kuilinda nchi na kutoa jibu la maamuzi kwa kitendo chochote cha uchokozi kutoka kwa maadui wake.

“Sisi katika Hizbullah hatutaki vita wala hatuvitafuti; lakini hatutasalimu amri, na tuko tayari kujilinda,” Sheikh Qassem alisema katika hotuba yake ya televisheni iliyotolewa kutoka mji mkuu wa Lebanon, Beirut, siku ya Jumatatu.

Aliongeza:

“Kuna tofauti kubwa kati ya kukabiliana na uchokozi na kuanzisha vita. Tuko tayari kwa ulinzi. Hatutakubali vitisho.”

Kiongozi wa Hizbullah alisema kuwa maadui hawatafanikiwa mbele ya harakati ya upinzani iliyo imara na yenye azma, pamoja na taifa kubwa na thabiti la Lebanon.

“Wanaweza kutuletea maumivu, lakini sisi pia tuna uwezo wa kuwaletea maumivu. Msidharau nguvu ya kujilinda wakati wake unapowadia.”

Sheikh Qassem alisisitiza kuwa kanuni ya msingi ni kutetea ardhi ya Lebanon, akisema kuwa kulinda nchi ni jukumu la kila raia.

Aliongeza kuwa Hizbullah inaunga mkono umoja wa kitaifa wa Lebanon, uhuru kamili wa nchi, pamoja na harakati za ukombozi, na inapinga aina zote za fitina na mgawanyiko.

“Tunaunga mkono kuimarishwa kwa Jeshi la Lebanon ili kulinda na kutimiza uhuru wa taifa, sambamba na mkakati wa usalama wa kitaifa na kutumia nguvu ya upinzani,” alisema.

Sheikh Qassem alihoji:

“Sisi ndio tunapaswa kuwauliza kwa nini hamlindi nchi, kwa nini hamkemei uchokozi, na kwa nini hamwisimamii kwa uthabiti wale wanaopinga uvamizi.”

Amesema serikali ya Lebanon inapaswa kubebeshwa lawama kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Israel, akisema kuwa mamlaka zinazotawala zinapaswa kuwajibishwa kwa sababu zilisaini makubaliano ya kusitisha mapigano na utawala wa Tel Aviv.

Aliikosoa vikali serikali kwa kufanya “kosa kubwa” kwa kuzingatia suala la kupokonywa Hizbullah silaha badala ya kukabiliana na uchokozi wa Israel, akisema mtazamo huo unahudumia malengo ya Israel.

Sheikh Qassem alisisitiza kuwa serikali ya Beirut inashiriki jukumu hilo pamoja na Hizbullah, Jeshi la Lebanon na taifa lote, akisema kuwa uvamizi popote pale unahitaji uwepo wa Hizbullah

Aliitaja Hezbollah kama:

“Hizbullah ni Harakati ya  kitaifa, Kiarabu, Kiislamu na ya kibinadamu, ambayo haiwezi kugawanywa.”

Aliongeza:

“Hatuko kwa ajili ya kutoa masharti ya kudhalilisha, wala kutekeleza maagizo ya uangalizi wa Marekani, kimataifa au Kiarabu, wala kutimiza matakwa ya kikatili ya Israel.”

Alisema kuwa serikali, kupitia mwenendo wake, inachangia kwa namna fulani tamaa ya utawala wa Israel kutokana na msururu wa maridhiano ya mara kwa mara.

“Ikiwa mnataka kusalimu amri, basi badilisheni katiba, kwa sababu kiini cha katiba ni mapambano na ulinzi kwa ajili ya ukombozi,” alisema akiwahutubia viongozi wa serikali ya Lebanon.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Qassem aliwataka wananchi wote wa Lebanon wasipuuze mauaji na ukatili wa Israel huko Gaza, wala juhudi zake za kunyakua Ukingo wa Magharibi, akisema kuwa Marekani inashiriki kikamilifu katika mipango hiyo yote.

“Israel ni chombo cha upanuzi kinachotaka kuikalia Palestina yote na eneo zima. Tunakabiliana na adui anayelenga kuangamiza binadamu na kuharibu miundombinu,” alisema.

Sheikh Qassem aliongeza kuwa licha ya Lebanon kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano ya Novemba 2024, Israel haijaheshimu hata moja ya ahadi zake.

3496445

Habari zinazohusiana
captcha