IQNA

Mashabiki wa Uhispania wachochea hasira za Lamine Yamal kwa chuki dhidi ya Uislamu

18:29 - April 01, 2026
Habari ID: 3482111
IQNA – Licha ya kuonywa, baadhi ya wafuasi wa timu ya taifa ya Uhispania walisikika wakipaza kauli ya kudhalilisha Uislamu wakati wa sare ya Jumanne dhidi ya Misri—kitendo kilichomkasirisha mshambuliaji wa Barcelona, Lamine Yamal.

Mechi hiyo, iliyokutanisha timu hizo mbili ambazo tayari zimefuzu Kombe la Dunia la 2026, haikuwa na matukio makubwa zaidi ya kadi nyekundu aliyopata Hamdy Fathy dakika chache kabla ya kumalizika, lakini gumzo kuu lilikuwa kauli ya chuki iliyoimbwa na mashabiki.

Katika dakika 10 za kwanza, mashabiki wa nyumbani walisikika wakisema maneno ambayo hutafsiriwa, “ruka, ruka, ruka, yeyote asiyeruka ni Mwislamu.”

Wimbo huo ulirudiwa mara kadhaa kipindi cha kwanza na mara baada ya kipindi cha pili kuanza cha mechii hiyo ambayo ilimalizika kwa sare tasa. Ujumbe uliokuwa ukionekana kwenye skrini kubwa uwanjani ulionya: “Tunawakumbusha kuwa sheria dhidi ya chuki katika michezo inakataza na kuadhibu ushiriki wa moja kwa moja katika vitendo vya ukatili, chuki na ubaguzi wa kikabila au wa kidini.”

Hata hivyo, mashabiki wengi walipokea ujumbe huo kwa kejeli na vilio vya mizaha.

Kwa mujibu wa The Athletic, nyimbo hizo mara nyingi huimbwa na mashabiki wa Uhispania dhidi ya timu pinzani, ingawa zinahusisha kauli zinazoweza kuwa za kibaguzi.

Misri, nchi yenye idadi kubwa ya Waislamu, ilikuwa mpinzani wao siku hiyo. Yamal, ambaye ana asili ya Morocco na ni Mwislamu anayefungamana na dini, aliripotiwa kuwa mchezaji pekee wa Uhispania ambaye hakupiga makofi kwa mashabiki baada ya mchezo; pia aliondoka uwanjani akiwa ameinamisha kichwa huku akiandamana na walinzi.

Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF) lilitoa tamko la kulaani kauli hizo, na kusema:

“RFEF inalani nyimbo hizo na imeagiza kutolewa ujumbe kupitia vipaza sauti uwanjani kukemea aina zote za ukatili katika soka.”

Kocha Luis de la Fuente, ambaye alimpa Yamal nafasi ya kwanza kuchezea taifa akiwa na umri wa miaka 16, alieleza maneno hayo “hayavumiliki” na akataka wahusika “kuondolewa kabisa katika jamii.”

Wachezaji wenzake – Pedri na kipa Joan Garcia – pia walionyesha masikitiko yao. Pedri alisema timu hiyo “imeshtushwa na kauli hizo,” akisisitiza kwamba “wote tunapaswa kushirikiana ili kudhibiti vitendo kama hivi.” Garcia, kwa upande wake, alisisitiza kwamba timu yao “inapinga kabisa aina yoyote ya ubaguzi.”

Uhispania, mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu kushinda Kombe la Dunia, itaanza kampeni yake kwa kucheza na Cape Verde tarehe 15 Juni mjini Atlanta. Katika Kundi H, watakabiliana pia na Saudi Arabia na Uruguay.

3496946

Habari zinazohusiana
captcha