
Mchezaji huyo kijana amesifiwa kuwa “kijana jasiri sana” baada ya kuonekana akipeperusha bendera kubwa ya Palestina kwenye basi la wazi la sherehe za Barcelona kufuatia kutwaa ubingwa wa La Liga.
Yamal mwenye umri wa miaka 18 alionekana akiwa ameshika bendera hiyo huku mabingwa hao wapya wa Hispania wakisalimia maelfu ya mashabiki wa Barca waliokuwa wamefurika mitaa ya mji wa Barcelona siku ya Jumatatu, saa chache baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Real Madrid katika El Clasico kuwahakikishia taji lao la pili mfululizo la ligi kuu.
Ingawa alikosa mchezo wa Jumapili kutokana na majeraha, Yamal alijiunga na wenzake katika gwaride la mabingwa siku iliyofuata.
Video za kitendo chake cha kuunga mkono wananchi wa Palestina zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, huku mashabiki wa soka, wachambuzi, wanaharakati na wachezaji wengi wakimpongeza nyota huyo kijana.
“Kwa baadhi ya watu huenda ikaonekana ni ishara ndogo tu, lakini hapa Gaza inagusa mioyo kwa namna ambayo maneno hayawezi kueleza,” aliandika Muhammad Akram, mwanafunzi wa Kipalestina mjini Gaza.
“Asante Lamine Yamal. Kutoka Gaza, unapendwa zaidi kuliko unavyodhani.”
Katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili iliyopita, bendera ya Palestina imekuwa ikipeperushwa katika mamia ya miji duniani na waandamanaji pamoja na wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina. Kwa wengi, hatua hiyo ni ishara ya mshikamano na wananchi wa Gaza ambao wamekuwa wakikabiliwa na mashambulizi ya mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel tangu Oktoba 7, 2023.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, zaidi ya Wapalestina 72,740 wameuawa tangu Oktoba 2023, huku watu 854 wakiripotiwa kuuawa hata katika kipindi kilichoitwa cha “usitishaji mapigano” kilichotiwa saini Oktoba mwaka jana.
Ingawa maandamano ya kuiunga mkono Palestina yamepungua tangu kuanza kwa usitishaji mapigano huo, wanaharakati wameendelea kupeperusha bendera ya Palestina katika mikusanyiko mikubwa ya umma ikiwemo matukio ya michezo na sherehe mbalimbali.
Yamal naye alitumia shamrashamra za ushindi wa Barcelona kuonyesha uungaji mkono wake kwa Palestina, huku baadhi ya wanaharakati wakisema kuwa kwa kitendo hicho kimoja ameweza kuongeza uelewa wa jambo hilo kuliko watu wengi wengine.
“Ukiwa na jukwaa, litumie. Ukiwa na sauti, sema ukweli,” aliandika mwanaharakati na mwandishi wa Lebanon, Dyab Abou Jahjah. “Hongera Lamine Yamal,” aliongeza.
Kocha mkuu wa Barcelona, Hansi Flick, alisema alizungumza na Yamal kuhusu tukio hilo.
“Nilizungumza naye na nikamwambia: ‘Ikiwa unataka kufanya hivyo, ni uamuzi wako, una umri wa kufanya maamuzi yako mwenyewe,’” kocha huyo Mjerumani aliwaambia waandishi wa habari Jumanne.
Baada ya sherehe hizo, mshambuliaji huyo wa Hispania alichapisha picha yake akiwa na bendera ya Palestina kwenye akaunti yake ya Instagram pamoja na picha nyingine za hafla hiyo.
Yamal ana wafuasi milioni 44.2 kwenye mtandao huo wa kijamii, ambapo chapisho lake lilipata zaidi ya “likes” milioni 5.3 pamoja na zaidi ya mara 100,000 za kushirikiwa katika masaa machache baada ya kuchapishwa.
3497444