
Msahafu (Nakala ya Qur'ani Tukufu) unaosadikiwa kuwa kuandikwa zaidi ya miaka 1,000, unaohifadhiwa katika Makumbusho ya Urithi wa Utamaduni wa Kiislamu na Kituo cha Mafunzo ya Al-Quran huko Narathiwat, Thailand, si tu kwamba una thamani kubwa ya kihistoria kwa Umma wa Kiislamu, bali pia unaashiria ustadi wa ustaarabu wa awali katika kutumia malighafi asilia kutengeneza Kitabu hiki Kitukufu.
Msahafu huo una uzito wa takriban kilo 50 na uliandikwa wakati wa enzi ya ukhalifa wa Bani Abbas. Umetengenezwa kwa kutumia kurasa 346 za ngozi za wanyama na wino wa asili wa kaboni, jambo linaloufanya kuwa miongoni mwa athari adimu na za thamani za kale za Kiislamu zinazohifadhiwa katika ukanda huo.
Afisa wa makumbusho hayo, Bw. Nik Ilham Nik Yusup, alisema kuwa athari hiyo ya kale zaidi ghalani mwao iliundwa kwa ufundi wa hali ya juu, ikitumia mamia ya ngozi za wanyama zilizosindikwa vyema ili kutengeneza kurasa imara kwa ajili ya kuandikia maneno ya Mwenyezi Mungu (SWT).
“Malighafi zote za msingi zilitoka moja kwa moja nchini Yemen, hususan kutoka eneo la Hadhramaut,” amesema.
Ikumbukwe kuwa Hadhramaut ni eneo lenye mafungamano makubwa ya kihistoria na kidini na Waislamu wa Pwani ya Afrika Mashariki.
Mbali na matumizi ya malighafi asilia, nakala hiyo inaashiria uwezo mkubwa wa jamii za awali za Kiislamu katika kutumia mazingira yao. Msahafu huo umeandikwa wote kwa mkono kwa kutumia Hati ya Kikufi ya kale, ukitumia wino wa kaboni uliotokana na vyanzo vya asili.
“Wazee wetu wa zamani walitumia vitu vilivyopatikana moja kwa moja kutoka kwenye maumbili asili. Mchanganyiko wa mti na magome ya mitende ulichomwa ili kutoa wino, kisha ukachanganywa na viungo vingine asilia kutoka mwituni,” alisema Bw. Nik Ilham.
Kwa kuwa Msahafu huu umeandikwa kikamilifu kwa vitu asilia vya kale, uhifadhi wake unahitaji umakini mkubwa na mbinu za kitamaduni zisizo na kemikali za kisasa. Kazi za kusafisha na ukarabati hufanyika kila baada ya miezi sita.
“Ngozi hizi ni laini na nyeti sana. Matumizi ya kemikali au vileo (alcohol) yanaweza kusababisha wino wa asili kupasuka, na umbile la kurasa linaweza kuharibika. Ndiyo maana tunatumia mbinu asilia za uhifadhi ili kulinda thamani na ukweli wa hazina hii adhimu,” aliongeza.
Alieleza kuwa safari ya Msahafu huo ilianzia Yemen kuelekea Visiwa vya Malay (Nusantara) wakati wa zama za mwanachuoni na mlinganiaji mashuhuri wa Kiislamu, Sheikh Jumadil Kubra.
Kwa mujibu wa maelezo yake, Msahafu huo ulihifadhiwa nchini Indonesia kwa zaidi ya miaka 500 kabla ya kupelekwa Narathiwat takriban miaka mitano iliyopita wakati wa janga la COVID-19.
“Ili kuhakikisha kuwa urithi huu usiokadirika wa ustaarabu wa Kiislamu unaendelea kulindwa, taratibu kali za usalama zimewekwa na wageni hawaruhusiwi kabisa kugusa athari hiyo,” alimalizia.
3497388