IQNA

Bodi ya kuhakikisha usahihi katika uchapishaji wa Qur’an Tukufu yazinduliwa Punjab, Pakistan

18:34 - May 19, 2026
Habari ID: 3482257
IQNA – Katika juhudi za kulinda Kitabu Kitukufu cha Qur’an dhidi ya makosa ya uchapishaji au mabadiliko yoyote ya kimaandishi, serikali ya mkoa wa Punjab nchini Pakistan imerejesha upya Bodi ya Qur’an ya mkoa huo. Serikali ya Punjab imeunda upya Bodi ya Qur’an ya Punjab kwa muhula wa miaka mitatu, ikisisitiza tena ahadi yake ya kulinda utukufu, usahihi, na uchapishaji mwafaka wa Qur’an Tukufu kwa mujibu wa miongozo ya kikatiba, kisheria, na kidini.

Katibu wa Idara ya Wakfu na Masuala ya Dini ya Punjab, Dkt. Ehsan Bhutta, amesema kuwa bodi hiyo mpya inaakisi azma ya serikali ya kuhakikisha uchapishaji na kurekodi kwa usahihi wa hali ya juu Qur’an Tukufu, huku ikihimiza mshikamano wa kidini miongoni mwa madhehebu mbalimbali. Ameongeza kuwa kuwajumuisha wanachuoni wanaoheshimika kutoka katika madhehebu zote za Kiislamu ni kielelezo cha umoja, heshima ya pande zote, na uwajibikaji wa pamoja katika kulinda Neno la Allah.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Idara ya Wakfu na Masuala ya Dini, serikali imeunda upya bodi hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 7(3) ikisomwa pamoja na Kanuni ya 7(1) ya Kanuni za Qur’an Tukufu (Uchapishaji na Kurekodi) za Punjab za mwaka 2011, baada ya kupata idhini kutoka kwa Waziri Kiongozi wa Punjab na baraza la mawaziri la mkoa huo.

Mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu, Maulana Zubair Hassan, atahudumu kama Mwenyekiti wa Bodi ya Qur’ani ya Punjab kwa kipindi cha mwaka mmoja. Dkt. Bhutta ameeleza imani yake kuwa bodi hiyo itatoa mwongozo wa kielimu, kisheria, na kidini kuhusiana na masuala ya uchapishaji na urekodi wa Qur’ani Tukufu.

Pia, amesifu mchango wa wanachuoni na kusema kuwa Serikali ya Punjab imedhamiria kuendeleza taasisi zinazohifadhi heshima na utakatifu wa Qur’ani Tukufu, huku ikihamasisha umoja miongoni mwa shule mbalimbali za fikra za Kiislamu.

Maafisa wamesema kuwa Bodi ya Qur’ani ya Punjab iliyoundwa upya itaendelea kufanya kazi ili kudumisha viwango vya hali ya juu katika uchapishaji na urekodi wa Qur’an Tukufu katika mkoa mzima, kwa ajili ya kuilinda hadhi ya Kitabu hicho kitukufu.

3497512

Habari zinazohusiana
Kishikizo: qurani tukufu pakistan
captcha