Mwandishi, mtafsiri, na mtafiti kutoka Lebanon, Haidar Hobbollah, amechapisha utafiti wa kina kuhusu historia na nyanja mbalimbali za maombolezo kwa Imam Hussein (AS) kwenye tovuti yake ya utafiti, hobbollah.com. Uchambuzi huu unachunguza jinsi Waislamu walivyoomboleza kufuatia kuuawa kwa mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) katika Vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 BK.
Hatua Tatu za Maombolezo
Kulingana na utafiti wa Hobbollah, mila za kumuomboleza Imam Hussein (AS) na mashahidi wa Karbala zinaweza kugawanywa katika hatua tatu katika kipindi cha karne tano za kwanza za Uislamu:
Huzuni kama Mwitikio wa Kimaumbile
Hobbollah anasema kuwa maombolezo kwa Imam Hussein (AS) hapo awali yalionyesha mwitikio wa kimaumbile wa binadamu wakati wa msiba. Anaandika, “Hata kama kusingekuwa na umuhimu wa kidini ulioshikamana na mila za maombolezo kwa Imam Hussein (AS), ingekuwa ni jambo la kawaida kwa watu kumlilia yeye na wale waliouawa shahidi pamoja naye wakati huo.”
Vyanzo vya kihistoria vinaonyesha kuwa mwaka wa kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (61 Hijiria / 680 BK) ulikuja kujulikana kama “Mwaka wa Huzuni.” Hobbollah anamnukulu Muwaffaq al-Khwarazmi (aliyefariki 568 H), ambaye alimnukuu mwanahistoria al-Bayhaqi akisema kuwa mwaka ambao Imam Hussein (AS) aliuawa, mwaka sitini na moja, uliitwa Mwaka wa Huzuni.
Kauli ya ‘Mwaka wa Huzuni’ inaashiria kuwa huzuni kwa Hussein (AS) ilikuwa jambo lililoenea, lisiloishia kwa watu wachache tu.
Mila za Awali za Maombolezo
Hobbollah anadokeza mifano kadhaa ya mapema ya maombolezo, ikiwa ni pamoja na simulizi zilizorekodiwa na Ibn Tawus (mwanazuoni wa Kishia wa karne ya 7 Hijiria) zinazoelezea hali ilivyokuwa mara baada ya vita. Simulizi hiyo inaelezea wanawake wakitoka nje ya mahema bila viatu na kulia, wakiomba kupelekwa mahali ambapo Imam Hussein (AS) aliuawa shahidi.
“Sitasahau kamwe Zaynab (SA), binti ya Ali (AS),” simulizi hiyo inaendelea, ikielezea jinsi alivyokuwa akiomboleza kwa ajili ya Hussein (AS) kwa sauti ya huzuni. Hobbollah anabainisha kuwa huu unawakilisha mkusanyiko wa kimaumbile wa maombolezo, ambao ni tofauti na sherehe za kisasa zilizopangwa, na anaonya kuwa simulizi kama hizo hazithibitishi kwamba vizazi vya awali vilichukulia maombolezo hayo kama ibada rasmi ya kidini.
Tofauti kati ya Maombolezo ya Maneno na Kujipiga
Utafiti unafanya ubaguzi muhimu wa kiisimu: “Maombolezo ni kitendo cha maneno (lamentation), wakati kupiga uso ni kitendo cha kimwili.” Hobbollah anabainisha kuwa pale Zaynab (SA) alipoomboleza kwa ajili ya Hussein (AS), haimaanishi lazima alijipiga usoni. Tofauti hii inahusu maandishi yote ya kihistoria yanayoelezea mila za maombolezo.
Mikusanyiko ya Kwanza ya Maombolezo Iliyopangwa
Hobbollah anamtaja Umm Salama, mke wa Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kama mmoja wa wanawake wa kwanza kufanya mkusanyiko wa maombolezo kwa ajili ya Imam Hussein (AS) mjini Madina. Maombolezo yaliendelea miongoni mwa watu wa Madina, ukoo wa Bani Hashim, na familia ya Mtume (SAW) kwa zaidi ya mwaka mmoja. Baadhi ya simulizi za kihistoria zinaonyesha kuwa walivaa nguo nyeusi za maombolezo.
Mtafiti huyo pia anarekodi mila za maombolezo za Tawwabin (wenye kutubu) walioinuka mwaka 65 Hijiria / 685 BK. Kulingana na mwanahistoria al-Tabari, walizuru kaburi la Imam Hussein (AS) alfajiri na kubaki hapo kwa mchana na usiku kucha, wakiswali na kuomba msamaha. “Watu walilia kwa sauti na kuomboleza pamoja,” al-Tabari anarekodi. “Hakukuwa na siku yenye vilio na maombolezo makubwa kuliko siku ile.”
3497902