Kwa mujibu wa Al-Kafeel, waombolezaji hao walianza msafara huo kwa miguu, huku sauti ya “Ya Hussein” ikitanda katika maeneo ya haram mbili takatifu za Imam Hussein (AS) na Hazrat Abbas (AS).
Rakdat al-Tuwairij ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya wanadamu duniani, na huandaliwa kila mwaka adhuhuri ya siku ya Ashura kwa kuhuisha kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussein (AS) pamoja na masahaba wake.
Mara nyingi ibada hiyo hufanyika katika sura ya msafara unaoanza baada ya Swala ya Adhuhuri.
Katika ada hii ya maombolezo, mazuwaru hupita kwa mbio nyepesi katika mitaa kwa umbali wa takriban kilomita 2 hadi 3 kuelekea kwenye Ataba tukufu ya Imam Hussein (AS), kwa kuenzi ile mbio iliyofanywa na binamu wa upande wa mama wa Hadhrat Abbas (AS) kutoka kijiji cha Tuwairij, kinachojulikana leo kama Al-Hindiya, kwenda Karbala baada ya tukio la Karbala.
Kwa ajili ya kushiriki maombolezo hayo, mazuwaru hukusanyika kwanza katika eneo la Qantara al-Salam katika kijiji cha Tuwairij karibu na Karbala, kisha huanza kuelekea kwa mwendo wa haraka hadi kwenye haram tukufu ya Imam Hussein (AS).
Njia hii ina urefu wa takriban kilomita 2, na katika safari hiyo waombolezaji hupaza sauti wakisema: “Labbayk Ya Hussein”, ikiwa ni jawabu la kimaana kwa mwito wa Imam Hussein (AS) siku ya Ashura aliposema: “Hal min nasirin yansuruna?” yaani, “Je, yuko yeyote atakayekuja kutunusuru?”
Wanahistoria wamesema kuwa maombolezo haya yalianza kwa mara ya kwanza mnamo 1855 au 1872 Miladia, na yaliandaliwa na mtu aliyeitwa Mirza Saleh Qazvini, ambaye alikuwa akiendesha majlisi za maombolezo nyumbani kwake katika eneo la Hendiyeh au Tuwairij katika siku kumi za kwanza za Muharram. Siku ya Ashura, waombolezaji walikuwa wakitoka nyumbani kwake na kuelekea kwenye haram tukufu.
Waislamu wa madhehebu ya Shia, pamoja na wengine duniani kote, huadhimisha kila mwaka kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussein (AS) katika mwezi wa Muharram wa kalenda ya Hijria, ambao ulianza tarehe 16 Juni mwaka huu.
Imam wa tatu wa Shia (AS) pamoja na kundi la ahli zake na masahaba wake waliuawa shahidi huko Karbala tarehe 10 Muharram (Ashura) mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia, mikononi mwa jeshi katili la mtawala dhalimu wa wakati huo, Yazid bin Muawiya.