IQNA

Bendera za Ashura zapeperushwa katika kote Ulaya

18:48 - June 26, 2026
Habari ID: 3482404
IQNA – Maelfu ya Waislamu wa Kishia na wapenzi wa Ahlul-Bayt (AS) katika miji mbalimbali ya Ulaya waliinua bendera za maombolezo ya Muharram na kupaza mwito wa “Labayka Ya Hussein”.

Kwa kuwasili kwa siku za Tasua na Ashura, yaani tarehe ya tisa na ya kumi ya mwezi wa Muharram, majlisi na maandamano ya maombolezo yalifanyika wiki hii katika miji tofauti barani Ulaya, yakieneza ujumbe wa uhuru, heshima na muqawama uliotokana na Karbala hadi katikati ya bara hili.

Barabara na vituo vya Kiislamu kuanzia London, Oslo na The Hague hadi Hamburg, Rome, Brussels na Stockholm, katika siku za karibuni vimepokea waombolezaji wa mataifa na lugha mbalimbali.

Walijikusanya chini ya bendera ya Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein (AS) na kuhuisha kumbukumbu ya tukio kubwa ambalo, hata baada ya kupita karne nyingi, linaendelea kuhamasisha watu wanaopigania uhuru duniani kote.

Moja ya maandamano makubwa na yenye kuvutia zaidi yalifanyika mjini Oslo, mji mkuu wa Norway. Takribani waumini 2,000 wa Ahlul-Bayt (AS) kutoka asili na mataifa tofauti walishiriki katika msafara uliojulikana kama “Ashuratug”, wakikumbuka msimamo, ushujaa na kujitoa muhanga kwa Imam Hussein (AS) na masahaba wake waaminifu katika ardhi ya Karbala.

Waandaaji wa hafla hiyo walieleza mahudhurio hayo makubwa kuwa ni miongoni mwa alama za neema na tawfiki ya kujikurubisha na Imam Hussein (AS), na wakaeleza matumaini yao kwamba ibada hii itaendelea kufanyika kwa uzuri na upana zaidi katika miaka ijayo.

Katika maandamano ya Oslo, pia zilisikika kaulimbiu za “Labayka Ya Khamenei”, na baadhi ya waombolezaji, huku wakiwa wamebeba bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, walionesha uhusiano uliopo kati ya ujumbe wa Ashura na muqawama wa kisasa dhidi ya dhulma, uvamizi na ubeberu.

Picha zilizotolewa kutoka hafla hiyo zinaonesha kuwa kaulimbiu za Imam Hussein (AS), sambamba na tamko la utii kwa kadhia ya muqawama, zilijaza mitaa ya mji mkuu wa Norway, huku bendera nyekundu na nyeusi za Ashura zikipeperushwa pamoja na bendera ya Iran.

Maandamano ya Ashura pia yalifanyika mjini The Hague, nchini Uholanzi. Baada ya kufanyika kwa majlisi ya maombolezo katika Kituo cha Kiislamu cha Mahfil Ali (AS), waombolezaji walipita katika mitaa ya mji huo wakiwa na bendera za Husseini, wakisoma tenzi za maombolezo, kupiga vifua na kupaza kaulimbiu za Ashura.

Mji wa Hamburg uliandaa maandamano ya Ashura siku ya Alhamisi. Aidha, Mahdiyeh ya Brussels nchini Ubelgiji iliendesha programu za siku kumi za kwanza za Muharram kwa ushiriki wa waombolezaji wanaozungumza Kifarsi pamoja na wapenzi wengine wa Ahlul-Bayt (AS). Mikusanyiko kama hiyo pia ilifanyika mjini Stockholm na katika miji mingine ya Uswidi, kwa lugha za Kifarsi, Kiarabu na Kiswidi, ikiwaleta pamoja vizazi mbalimbali vya Waislamu wahamiaji chini ya bendera ya Bwana wa Mashahidi (AS).

Maandamano makubwa ya Ashura pia yamepangwa kufanyika mjini Berlin siku ya Jumamosi. Waandaaji wamewaalika watu wote wanaopinga dhulma kujiunga na msafara huo na kupaza ujumbe wa milele wa “Hatutakubali fedheha kamwe” katika mji mkuu wa Ujerumani.

Nchini Uingereza, Kituo cha Kiislamu cha England pamoja na misikiti, hussainiya na vituo vya kidini kadhaa mjini London na miji mingine vimeendesha mikusanyiko ya Tasua na Ashura. Maandamano makuu ya Ashura nayo yanatarajiwa kufanyika katikati ya jiji la London siku ya Ijumaa.

3497976

Habari zinazohusiana
captcha