Akizungumza na IQNA, Reza Moammemi Moqaddam, mkurugenzi mkuu wa Idara ya Utamaduni na Masuala ya Kijamii katika Taasisi ya Wakfu na Misaada, alisisitiza nafasi ya kipekee ya Qur’ani Tukufu katika maandamano ya mamilioni ya watu ya Arbaeen. “Arbaeen si mkusanyiko mkubwa tu wa wanadamu, bali ni taswira hai ya mafundisho ya Qur’ani kwa vitendo. Ni dhihirisho la kujenga umma kwa misingi ya Qur’ani, umoja wa Kiislamu, na kusimama imara dhidi ya dhulma,” alisema kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa Qur’ani Tukufu ina nafasi isiyoweza kuchukuliwa na kitu kingine katika matembezi haya, kwani ni mwongozo wa kiakili, kimaadili, na wa kuunganisha kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na kwa Ummah mzima wa Kiislamu.
Katika njia ya matembezi ya kidini ya Arbaeen, alieleza, sauti ya Qur’ani ndiyo inatawala — usomaji wa Qur’ani unasikika kila kona, vikao vya kujifunza Qur’ani huandaliwa njiani kuelekea Karbala, na aya za jihadi, subira, na kusimama kwa haki hurindima kwenye kauli mbiu na mimbari.
“Aya tukufu za Qur’ani husikika kwa nguvu katika njia kutoka Najaf hadi Karbala. Kauli mbiu za wafanyaziara wa Arbaeen zimejaa mafundisho ya Qur’ani, maandamano hufufuliwa kwa usomaji wa nuru, na vijana hulelewa kwa misingi ya Qur’ani ndani ya moyo wa harakati hii tukufu,” alisema. Afisa huyo pia aligusia mipango maalumu ya Qur’ani inayoratibiwa na taasisi yao katika njia ya Arbaeen, ikiwa ni pamoja na vikao vya Qur’ani, usomaji wa aya takatifu kila siku katika mahema ya Mwkib, mpango wa usomaji wa Qur’ani kwa nia ya hawabu kwa mashahidi, vipindi vifupi vya tafakari juu ya aya za Qur’ani, na ushauri wa Qur’ani kwa mahujaji.
Aidha, alitangaza uzinduzi wa vikao maalumu vya Qur’ani kwa wageni wasiokuwa Wairani huko Karbala na Najaf, na kusema: “Kupitia programu hizi, tutageuza Arbaeen kuwa uwanja wa jihadi ya kubainisha Qur’ani, na tutatangaza kwa sauti kuwa Ummah wa Qur’ani unasimama dhidi ya dhulma, upotoshaji, na kiburi cha mabeberu.” Arbaeen ni tukio la kidini linaloenziwa na Waislamu wa Shia siku ya arobaini baada ya siku ya Ashura, kukumbuka kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (A.S), mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W) na Imamu wa tatu wa Shia. Ni moja ya mjumuiko mkubwa zaidi duniani inayofanyika kila mwaka, ambapo mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, pamoja na baadhi ya Masunni na watu wa dini nyingine, hutembea kwa miguu kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen itakuwa tarehe 14 Agosti. Takriban Wairani milioni nne wanatarajiwa kushiriki katika matembezi haya ya Arbaeen mwaka huu, InshaAllah. 3493956