Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa na Waislamu hasa wa madhehebu ya Shia katika siku ya arubaini baada ya Siku ya Ashura, ambayo ni kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na imamu wa tatu wa Shia katika mapambano ya Karbala mwaka 61 Hijria
Ni miongoni mwa safari kubwa zaidi za kila mwaka duniani, huku mamilioni ya Waislamu na hata wasiokuwa Waislalmu wakitembea kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen ilisadifiana na tarehe 25 Agosti.
Uhusiano kati ya matembezi ya ya Arbaeen na mafundisho ya Qur'ani unaweza kuangazia katika viwango kadhaa:
1- Kumuabudu na kumkaribia Mwenyezi Mungu
- Kutembelea makaburi ya mawalii wa Mwenyezi Mungu. Qur'ani Tukufu inasisitiza kuzuru makaburi ya mawalii wa Mwenyezi Mungu na safari ya Arbaeen inatekeleza mafundisho haya ya Qur'ani.
- Kumwabudu Mwenyezi Mungu katika mahali patakatifu. Kutembelea Karbala kama sehemu takatifu kunatoa fursa ya kumwabudu Mwenyezi Mungu na kumkaribia zaidi, jambo ambalo linaendana na aya za Qur’ani kuhusu kumwabudu Mungu katika maeneo matakatifu.
2- Uvumilivu na ujasiri
- Mtihani wa uvumilivu. Wafanyaziara wa Arbaeen wanakabiliwa na matatizo na masaibu mengi njiani, ambayo yanawatahini kuhusu uthabiti na uimara wao. Haya yanawiana na aya za Qur’ani kama Aya ya 10 ya Suratul Zumar zinazobainisha malipo makubwa kwa wenye subira: “Mwenyezi Mungu atawalipa walio subiri bila ya kuhisabu.
3- Usafi wa Nia
Kuabudu Mwenyezi Mungu kwa nia safi. Qur’ani Tukufu inasisitiza umuhimu wa Ikhlas (usafi wa nia) katika matendo ya ibada. Wafanyaziara wa Arbaeen hutembea kuelekea Karbala kwa nia safi ya kufikia hadhi ya Qurb (ukaribu na Mungu).
4- Umoja na usawa
- Umoja wa Waislamu. Maandamano au matembezi ya Arbaeen ni ishara ya umoja na udugu wa Waislamu. Haya yanawiana na aya za Qur'an zinazoitaja umoja wa Kiislamu, kama Aya ya 103 ya Surah Al Imran: "Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu, wala msitawanyike."
5- Kupambana na dhulma na dhulma
- Mwamako wa Imam Husein (AS) ulikuwa dhidi ya dhulma na hivyo matembezi ya Arbaeen ni kutangaza upya mfunganoa na mwamako huu unaowiana na aya za Qur’ani Tukufu zinazotaka kusimama kidete dhidi ya dhulma na madhalimu.
6- Mapenzi ya Ahl-ul-Bayt (AS)
- Qur'ani Tukufu inasisitiza haja ya kuwapenda Ahl-ul-Bayt (AS) na matembezi ya Arbaeen ni dhihirisho la upendo huu.
7- Kujiboresha na kutakasa nafsi
-Kuacha dhambi na kumkaribia Mwenyezi Mungu. Matembezi ya ya Arbaien ni fursa ya kutubia, kuacha madhambi na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, sambamba na aya za Qur’ani zinazohusu toba.
Kwa hiyo, matembezi ya Arbaeen ni ibada ya kina ambayo ina mafungamano ya kina na mafundisho ya Qur’ani. Ni dhihirisho la mafundisho ya Qur'ani kama imani, subira, Ikhlas, umoja na kupiga vita dhulma na ukandamizaji.
3489730