IQNA

Arbaeen 1446

Msafara wa Qur’ani wa Chuo Kikuu cha Al-Mustafa waelekea Iraq kushiriki Arbaeen

22:55 - August 20, 2024
Habari ID: 3479305
IQNA - Kundi la wanaharakati wa Qur'ani wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa wamelekea Iraq Jumatatu jioni kushiriki katika matembezi ya Arbaeen ya Imam Hussein (AS).

Wanajumuisha maqari na wahifadhi Qur'ani na wanachama wa kikundi cha Tawasheeh cha Biza'at al-Mustafa.

Hujjatul Islam Mohammad Hossein Rafiei, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Qur'ani na Hadithi ya chuo hicho ameiambia IQNA kwamba msafara huo unajumuisha washiriki 30 na utaendesha programu za Qur'ani na shughuli za kueneza Uislamu.

Alisema programu hizo ni pamoja na usomaji wa Qur'ani, usomaji wa Tarteel, Tawasheeh, Adhana na mashairi ya maombolezo.

Kujibu maswali ya Qur'ani ya wanaoshiriki matembezi ya Arbaeen pia ni katika ajenda ya kundi hilo, alisema.

Msafara huo unajumuisha maprofesa na wanafunzi wa chuo hicho kutoka nchi mbalimbali, zikiwemo Pakistan, India, Nigeria, Afghanistan, Mali, Burkina Faso, Tajikistan na Iraq, alibainisha.

Hujjatul Islam Rafiei ameongeza kuwa, kundi hilo linashiriki katika safari hiyo ya kiroho kwa lengo la kutoa huduma za Qur'ani kwa wafanyaziara wa Arbaeen.

Mjumuiko wa maombolezo ya Arbaeen ni mojawapo ya mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani.

Maadhimisho ya Arbaeen hufanyika siku ya 40 baada ya Ashura, ukumbusho adhimu wa kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu  wa Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliuawa shahdi na jeshi katili la la Yazid katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia.

Kila mwaka mamilioni ya Mashia na pia idadi kubwa ya wasiokuwa Mashia humiminika  katika mji Karbala nchini Iraq, mji ulipo Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS) ili kushiriki katika shughuli za maombolezo. Wafanya ziara, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri mamia ya kilomita kwa miguu hadi mji mtakatifu wa Karbala. Arbaeen ya mwaka huu inatarajiwa kuanguka mnamo Agosti 25, kulingana na kuonekana kwa mwezi.

Harakati ya mapambano ya Imam Hussein (AS) dhidi ya dhulma na ufisadi wa utawala wa Bani Umayya ilijaa hamasa, kujitolea na kusabilia kila kitu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, haki na uadilifu, na kwa sababu hiyo imegusa sana nyoyo za Waislamu na hata wapenda haki na kweli wasio Waislamu. Harakati hiyo ya Imam Hussein (AS) inaendelea kuibua vuguvugu na hamasa ya aina yake ndani ya nafsi za wapenzi wa mtukufu huyo.

3489575

 

 

Habari zinazohusiana
Kishikizo: qurani tukufu arbaeen
captcha