IQNA

Italia yazindua hati ya kitaifa ya mazungumzo ya kati ya dini mbali mbali

17:47 - June 29, 2026
Habari ID: 3482416
IQNA – Wawakilishi wa dini na madhehebu mbalimbali nchini Italia wameandaa hati ya kwanza ya kitaifa kwa ajili ya kuimarisha mazungumzo ya kati ya dini.

Kwa mujibu wa italiatelegraph, hati hiyo ni hatua ya kihistoria inayokusanya pamoja makundi 15 ya kidini nchini humo. Inafungua awamu mpya ya ushirikiano na mshikamano kwa ajili ya amani, uthabiti wa kijamii na kuimarisha maadili ya uraia.

Mnamo tarehe 25 Juni 2026, jiji la Roma lilishuhudia kutiwa saini rasmi kwa hati iitwayo “Njia ya Italia kwa Mazungumzo ya Kati ya Dini”, ambayo ni hati ya kwanza ya kitaifa ya aina yake. Hati hiyo iliunganisha jumuiya kumi na tano za kidini nchini Italia katika waraka mmoja wa pamoja. Tukio hilo lilifuata miaka mitatu ya mikutano na majadiliano yaliyoanza mwaka 2023, yakilenga kujenga utamaduni wa mazungumzo, kukuza heshima ya pande zote na kupanua ushirikiano kati ya taasisi za kidini kwa manufaa ya jamii ya Italia.

Hati hiyo imejengwa juu ya maono yanayothibitisha kuwa utofauti wa dini ni thamani chanya kwa jamii ya Italia, na kwamba mazungumzo ya kati ya dini ni nyenzo muhimu katika kujenga uaminifu, kuimarisha maisha ya pamoja na kupambana na chuki, misimamo mikali na ubaguzi.

Pia hati hiyo inajumuisha mkusanyiko wa misingi na ahadi za vitendo zinazolenga kugeuza mazungumzo ya kati ya dini kuwa utaratibu endelevu wa kitaasisi unaotegemea ushirikiano na heshima ya pande zote. Lengo lake ni kutafsiri dhamira ya pamoja katika mipango na miradi ya vitendo itakayohudumia jamii ya Italia.

Kituo cha Utamaduni wa Kiislamu cha Italia pamoja na Msikiti Mkuu wa Roma ni taasisi mbili za Kiislamu zilizoshiriki katika tukio hilo la kitaifa, na rais wa kituo hicho, Sheikh Naim Nasrallah, alitia saini hati hiyo kwa niaba ya taasisi hiyo.

Naye Sheikh Nader Akkad, Imamu wa Msikiti Mkuu wa Roma, alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni matunda ya miaka mitatu ya mikutano, mazungumzo na kazi endelevu. Akieleza fahari yake kushiriki katika mchakato uliosababisha kutiwa saini kwa hati hiyo, alibainisha kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa awamu mpya ya ushirikiano kati ya wafuasi wa dini mbalimbali, si mwisho wa safari.

Baada ya hafla ya utiaji saini, Rais wa Italia Sergio Mattarella aliwapokea wawakilishi wa makundi ya kidini yaliyotia saini hati hiyo katika Ikulu ya Quirinale, ambapo alipokea nakala rasmi ya waraka huo. Hatua hiyo inaonesha uungwaji mkono rasmi wa serikali ya Italia kwa mazungumzo ya kati ya dini, ambayo inaona kuwa ni nguzo muhimu ya mshikamano wa kijamii na kukuza utamaduni wa kuishi pamoja.

Hati hii ni waraka wa kwanza wa pamoja wa kitaifa uliowaunganisha viongozi na taasisi nyingi za kidini nchini Italia chini ya maono ya pamoja ya mazungumzo na ushirikiano. Inaweka msingi wa hatua mpya ambapo mazungumzo ya kati ya dini yanakuwa mfumo wa kudumu wa kitaasisi unaosaidia kukabiliana na changamoto za kijamii na kuimarisha maadili ya amani, heshima na ushirikiano kati ya sehemu zote za jamii ya Italia.

Italia ina idadi ya watu wapatao milioni 59, ambapo takriban Waislamu milioni 2.8 wanaishi nchini humo, sawa na karibu asilimia 4.7 ya jumla ya wakazi. Msikiti Mkuu wa Roma na Kituo cha Utamaduni wa Kiislamu cha Italia ni miongoni mwa taasisi muhimu zaidi za Kiislamu nchini humo, zikichukua nafasi muhimu katika mazungumzo na serikali pamoja na taasisi nyingine za kidini, na katika kuimarisha uwepo wa Waislamu katika maisha ya umma.

3498004

captcha