IQNA

Wairaki watembea kwa miguu hadi Najaf kwa mnasaba wa kukumbuka kifo cha Mtume Muhammad SAW

21:19 - October 15, 2020
Habari ID: 3473262
TEHRAN (IQNA) - Idadi kubwa ya Wairaki wametembea kwa miguu kutoka mji wa Karbala kuelekea Najaf kwa lengo la kushiriki katika shughuli ya maombolezo na kukumbuka tukio chungu la kuaga dunia Mtume Muhammad SAW.

Kwa mujibu wa taarifa wanaoshiriki katika matembezi hayo ni wale ambao walikuwa wamefika Karbala kushiriki katika hafla ya Arubaini ya Imam Hussein AS. Matemebezi hayo yalianzia katika Haram ya Imam Hussein AS na wameelekea katika Haram ya Imam Ali AS mjini Najaf

Wakati huo huo, Harakati ya al Hashdul Shaabi ya Iraq imetangaza kuwa inatekeleza mpango wa usalama na kutoa huduma kwa maelfu ya Waislamu watakaoshiriki katika shughuli ya maombolezo na kukumbuka tukio chungu la kuaga dunia Mtume Muhammad SAW utakaosimamiwa na askari elfu 12 wa harakati hiyo hususan katika mji mtakatifu wa Najaf.

Kesho Ijumaa inasadifiana na tarehe 28 Mfunguo Tano Safar ni siku ya kumbukumbu ya kuaga dunia Mtume Muhammad SAW na vilevile kumbukumbu ya siku ya kuuawa shahidi mjukuu wake, Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib AS

Naibu Mkuu wa harakati ya al Hashdul Shaabi, Adnan al Najjar amesema leo kwamba, harakati hiyo imejiandaa kutoa huduma kwa Waislamu wanaokwenda kufanya ziara sambamba na kushiriki katika maombolezo ya kumbukumbu ya kifo cha Mtume Muhammad SAW.

Wakati huo huo kamanda ya Operesheni ya al Furat al Ausat ya al Hashdul Shaabi, Ali al Hamdani amesema kuwa, askari wa Divisheni ya Imam Ali AS na Brigedi ya Ali Akbar wakishirikiana na idara mbalimbali wamepelekwa katika njia zote za kuingia katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya kudhamini usalama na kutoa huduma makhsusi kwa Waislamu wanaoshiriki kwenye kumbukumbu ya siku ya kuaga dunia Mtume wa Mwa Mwenyenzi Mungu, Muhammad SAW.

 

3929502

captcha