IQNA

21:34 - January 15, 2021
News ID: 3473558
TEHRAN (IQNA)- David Beasley Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (WFP) amesema kuwa uamuzi Marekani dhidi ya harakati ya Ansarullah ya Yemen ni sawa na kutolewa hukumu ya kifo kwa Wayemen wasio na hatia.

Ikiwa ni katika juhudi zake za kuunga mkono muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen, Marekani imechukua hatua ya kuiwekea vikwazo harakati ya Ansarullah ambayo inaongoza Yemen. Hatua hiyo ambayo imechukuliwa katika siku za mwisho za utawala wa Rais Trump huko White House imekabiliwa na radiamali kali ya Umoja wa Mataifa.

Martin Griffiths, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen, Mark Lowcock, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu na David Beasley, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (WFP)  katika kikao cha Baraza la Usalama kilichoandaliwa siku ya Alkhamisi kwa ajili ya kujadili suala la Yemen, wameitaka serikali ya Marekani iliondoe jina la Ansarullah katika orodha ya makundi yanayotuhumiwa na serikali hiyo kuwa ni ya kigaidi.

 Kwa mujibu wa Griffiths kuwekwa jina la kundi hilo la mapambano ya Kiislamu katika orodha ya makundi ya kigaidi kutaeneza njaa huko Yemen na kufanya kuwa ngumu shughuli za mashirika ya ufikishaji misaada ya kibidamu nchini humo. David Beasley pia amesema kuwa uamuzi huo wa Marekani dhidi ya Ansarullah ni sawa na kutolewa hukumu ya kifo dhidi ya mamilioni ya watu wasio na hatia nchini Yemen.

Serikali ya Marekani imekataa ombi hilo la Umoja wa Mataifa la kuondolewa jina la Ansarullah katika orodha ya makundi ya kigaidi licha ya maonyo mengi ambayo yametolewa na mashirika na viongozi wa kimataifa kuhusu taathira mbaya za hatua hiyo. Akitetea hatua hiyo mbovu ya serikali ya Trump, Richard Mills, Naibu Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amedai kuwa jamii ya kimataifa inapasa kuunga mkono hatua hiyo, iwapo inataka kuona eti mkondo sahihi wa kisiasa ukichukuliwa huko Yemen.

Ni wazi kuwa baada ya kuona kwamba Saudi Arabia imeshindwa kufikia natija yoyote ya maana katika vita vyake vya kichokozi vya miaka 6 huko Yemen, saa Marekani imeamua kuingilia yenyewe moja kwa moja vita hivyo na kwa kuliwekea vikwazo vya kidhalimu kundi la Ansarullah inataka kuzuia kwa kila njia kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Yemen. Kwa kutumia mbinu hiyo, Marekani inakusudia kuwalazimisha wananchi wa Yemen wasalimu amri mbele ya matakwa haramu ya Saudi Arabia. Marekani imekuwa na mchango mkubwa zaidi katika vita vya Yemen ambavyo vilianza mwezi Machi 2015 ambapo imekuwa ikiupa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia kila aina ya misaada ya kilojistiki, habari za siri za kiusalama na kijeshi. Mashambgulio ya kinyama yanayofanywa na muungano huo yameharibu kabisa miundombinu ya Yemen na kuzidisha umasikini wa kupindukia, njaa na magonjwa sugu katika nchi hiyo masikini zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa Yemen ndiyo nchi inayokabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani. Watu wapatao milioni 22 ambao ni asilimia 75 ya jamii ya nchi hiyo wanahitajia misaada ya dharura ya kibinadamu. Kati ya hao, watu milioni 8.4 hawajui watapata wapi mlo wao wa baadaye.

Ni wazi kuwa muungano wa vita unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen haungeweza kuendesha vita hivyo vya muda mrefu bila ya kuwepo misaada ya dhahiri na ya siri ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani.

3473705

Tags: yemen ، ansarullah ، waislamu
Name:
Email:
* Comment:
* captcha: