IQNA

Waislamu India

Mahakama India yaaidhinisha ibada za Kihindu ndani ya Msikiti wa kihistoria

20:01 - February 02, 2024
Habari ID: 3478291
IQNA - Msikiti wa Gyanvapi huko Varanasi, ni eneo la kihistoria iliyojengwa katika karne ya 17, umekuwa kitovu cha hivi punde katika mzozo wa muda mrefu wa kisheria kati ya Wahindu na Waislamu nchini India.

Baadhi ya Wahindu wenye misimamo mikali wanadai kuwa msikiti huo uko eneo la hekalu takatifu kwa mujibu wa imani yao.

Siku ya Jumatano, mahakama ya wilaya ya Varanasi iliwaruhusu Wahindu kuabudu katika sehemu ya chini ya msikiti, ambapo sanamu ya mmoja wa miungi ya Kihindu, Shiva, inadaiwa kupatikana.

Mahakama iliamuru wasimamizi wa eneo hilo wafanye mipango ya maombi hayo ndani ya wiki moja. Upande wa Waislamu, hata hivyo, ulipinga agizo la mahakama na kuwasilisha ombi la marekebisho katika Mahakama Kuu ya Allahabad, kutaka kuzuiwa kwa uamuzi huo, kwa mujibu wa Wion News.

Waislamu hapo awali walienda Mahakama ya Juu kwa ajili ya kusikilizwa kwa dharura, lakini kesi ilielekezwa kwa Mahakama Kuu ya Allahabad.

Amri hiyo ya mahakama ilitokana na ripoti ya Taasisi ya Archaeological Survey of India (ASI), ambayo ilifanya uchunguzi wa eneo hilo mwezi uliopita na kudai kuwa ilipata ushahidi wa hekalu la Kihindu chini ya msikiti huo.

Ripoti hiyo ilidai kuwa muundo wa awali ulibomolewa na sehemu zake zilitumika katika ujenzi wa msikiti uliokuwepo.

Msikiti wa Gyanvapi ni miongoni mwa maelfu ya misikiti ambayo imekuwa ikilengwa na Wahindu wenye misimamo mikali ambao wanataka kuchukua udhibiti wa maeneo ambayo wanaamini yalijengwa juu ya mahekalu ya zamani wakati wa utawala wa Mughal.

Kesi maarufu zaidi ilikuwa Msikiti wa Babri huko Ayodhya, ambao ulibomolewa na genge  la Wahindu wenye misimamo mikali mnamo 1992, na kusababisha ghasia zilizoua zaidi ya watu 2,000. Mnamo mwaka wa 2019, Mahakama ya Juu iliamuru eneo hilo la Waislamu likabidhiwe Wahindu, na kufungua njia ya ujenzi wa hekalu la Ram, ambalo lilizinduliwa mwezi uliopita.

Kesi ya Msikiti wa Gyanvapi imeibua wasi wasi juu ya hatima ya maeneo mengine ya ibada ya Waislamu nchini India, pamoja na uwezekano wa kutokea vurugu na machafuko ya jamii.

Msikiti huo uko Varanas, ngome ya chama tawala chenye misimamo mikali ya Bharatiya Janata Party (BJP) cha Waziri Mkuu Narendra Modi.

captcha