IQNA

Rambirambi

Viongozi wa dunia wakiwemo wa Afrika waendelea kumuomboleza kifo Raisi

17:28 - May 20, 2024
Habari ID: 3478855
IQNA-Viongozi wa dunia wameendelea kutuma salamu za rambi rambi kufuatia kufa shahidi katika ajali ya helikopta jana Seyyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, Hujjatul Islam wal Muslimin Al Hashem, mwakilishi wa Waliul Faqih katika Mkoa wa Azabajan Mashariki, Malik Rahmati, Gavana wa Azabajani Mashariki na wote waliokuwa katika msafaraha huo.

Rais William Ruto wa Kenya amemuomboleza mwenzake wa Iran Ebrahim Raisi aliyefariki dunia katika ajali ya helikopta Jumapili, Mei 19.

Katika taarifa yake kupitia ukurasa wa kijamii wa X, Ruto ametuma rambirambi na mshikamano wake na watu wa Iran katika wakati huu mgumu.

Ruto amemkumbuka Rais Raisi kama kiongozi asiye na woga na mtumishi wa umma aliyejitolea na kazi iliyotukuka katika utumishi wa umma.

Ruto amesema: "Napenda kutoa rambirambi zangu za dhati na mshikamano na watu wa Iran katika wakati huu mgumu,"

Amemtaja kama kiongozi thabiti aliyejitolea kwa mambo ambayo aliamini na alijaribu kuinua msimamo wa Iran katika jukwaa la kimataifa.

Ruto amebainisha kuwa Kenya na Jamhuri ya Iran zina uhusiano wa kidugu, huku akiashiria ziara ya Raisi nchini Kenya Julai 2023 ikiwa ni safari ya kwanza kabisa barani Afrika kama Rais.

Ruto ameongeza kuwa: "Tunapowapa pole wananchi wa Iran, tunamuomba Mwenyezi Mungu awafariji wananchi wa Iran."

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini leo Jumatatu ametoa salamu za rambirambi kufuatia ajali ya helikopta iliyopelekea kufa shahidi Rais wa Iran Ayatullah Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na maafisa wengine.

Katika taarifa, Ramaphosa amesema: "Huu ni mkasa usio wa kawaida, usiofikirika ambao umechukua uhai wa kiongozi wa kipekee wa taifa ambalo Afrika Kusini ina uhusiano mzuri nalo na ambaye tulipata heshima kubwa kumkaribisha kwenye mkutano wa BRICS huko Johannesburg mwaka 2023."

Ramaphosa amesema nchi yake inaungana na Iran katika wakati huu wa maombolezo, na kwamba mawazo yake yako pamoja na familia zilizoathirika pamoja na uongozi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Vile vile ametoa salamu za rambirambi kwa Kiongozi Muadhamu wa Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, pamoja na serikali na watu wa Jamhuri ya Kiislamu.

Rais wa Russia Vladimir Putin amemsifu Raisi kama "mwanasiasa mashuhuri" na kusema kifo chake ni "hasara isiyoweza kufidiwa."

Russia, India na China

"Raisi alikuwa mwanasiasa mashuhuri ambaye katika maisha yake yote alijitolea kutumikia nchi yake," Putin amesema katika barua kwa Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Rais Xi Jinping wa China naye pia ametuma salamu zake za rambirambi, akisema "kifo cha kutisha" cha mwenzake wa Iran ni "hasara kubwa kwa watu wa Iran."

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi pia amesema "amehuzunishwa sana na kushtushwa na kifo cha kusikitisha" cha rais wa Iran.

Pakistan, UAE, Uturuki

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif ametangaza siku ya maombolezo ya kitaifa "kama ishara ya heshima kwa Rais Raisi na viongozi wenzake na pia kwa ajili ya mshikamano na Ndugu wa Iran."

Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan amesema nchi yake "inasimama katika mshikamano na Iran katika wakati huu mgumu."

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemuelezea Raeisi kama "mwenzake na kaka yake."

Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani ametuma "rambirambi zake za dhati kwa serikali na watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran" kufuatia tukio hilo chungu.

Katika jumbe mbili tofauti zilizotumwa kwa rais wa mpito wa Iran Mohammad Mokhber, Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz Al Saud na Mwanamfalme Mohammed bin Salman wametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Raisi na maafisa aliokuwa ameandamana nao.

Rais wa Syria Bashar al-Assad amesema "kujitolea kwa mwenzake wa Iran kwa kazi yake" kumemfanya akufe shahidi katika njia ya Uislamu.

Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi amehuzunishwa na tukio hilo na kutangaza "mshikamano wa Cairo na uongozi na watu wa Iran."

Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim pia amesema Raisi "alionyesha dhamira ya kina kwa ustawi wa watu wake na hadhi ya taifa lake, ambayo inawakilisha ustaarabu wa fahari na tajiri unaojikita katika misingi ya Uislamu."

Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan Ilham Aliyev ambaye alikutana na Rais Raisi kabla ya ajali katika mpaka wa nchi mbili wakati wa kuzindua bwawa amesema "Watu wa Iran wamempoteza mwanasiasa mashuhuri ambaye aliitumikia nchi yake kwa kujitolea na uaminifu maisha yake yote."

"Katika siku hii ya huzuni, ninamuomba Mwenyezi Mungu awape subira na ujasiri marafiki na ndugu wa Iran."

3488413

Habari zinazohusiana
captcha