IQNA

Siasa

Kiongozi Muadhamu: Baraza la Wanazuoni Wataalamu, ni shina la demokrasia ya Kiislamu

16:16 - May 21, 2024
Habari ID: 3478858
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei amelitaja Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa shina na kitovu cha demokrasia ya Kiislamu.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo katika ujumbe alioutoa kwa mnasaba wa kuzinduliwa Baraza la Sita la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu, lililoanza rasmi kazi zake leo Jumanne.

Katika ujumbe wake huo, Kiongozi Muadhamu ametoa mwito kwa dhamiri zilizoamka za walimwengu kutafakari juu ya mpango mpana, thabiti, nadhifu, wa kuvutia na wa kustaajabisha wa mfumo wa Kiislamu, huku wakizingatia pia juu ya ukweli mchungu wa mifumo ya uongozi inayopinga au kujiweka mbali na dini. 

Baraza la Sita la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu limeanza rasmi kazi zake leo kwa kuhudhuriwa na akthari ya wajumbe wapya wa baraza hilo. Ikumbukwe kuwa, uchaguzi wa baraza hilo ulifanyika Machi mwaka huu sambamba na wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).

Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa, uchaguzi ni jambo muhimu kwa nchi na wananchi, na ni ishara ya ushiriki wa wananchi na kupewa fursa ya kufanya maamuzi yao, na kudhihirisha irada zao kwa taifa lao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza bayana kuwa, katika mfumo wa Kiislamu, malengo huwa matakatifu. Amebainisha kuwa, kumteua Kiongozi Muadhamu kwa mujibu wa viwango na vigezo vya Kiislamu ni jukumu la Baraza la Wanazuoni Wataalamu, ambalo lenyewe huchaguliwa na wananchi, na hii ndiyo alama na kielezo cha wazi zaidi cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kadhalika Ayatullah Khamenei ameashiria vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa Marekani huko Gaza na kusisitiza kuwa: Uungaji mkono wa serikali eti za kiliberali za Wamagharibi kwa Israel umefichua maana halisi ya 'uhuru' na 'haki za binadamu' kwa mujibu mataifa hayo.

Kwa mara nyingine tena, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa salamu za rambirambi kufuatia kufa shahidi Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ujumbe alioandamana nao, huku akimuomba Allah Awaghufirie na Awamiminie baraka zake.

4217363

Habari zinazohusiana
captcha