IQNA

Arafa ni siku yenye upepo mwanana wa rehema za Mwenyezi Mungu

22:14 - June 14, 2024
Habari ID: 3478967
IQNA- siku ya Arafa yaani mwezi Tisa Mfunguo Tatu Dhulhija ni fursa kwa ajili ya dua na kuomba maghufira kwa Waislamu wote wawe katika Hija au wale ambao hawakupata taufiki ya Hija..

Mahujaji wanapoingia katika ardhi ya Arafa hupata kumbukumbu ya mafundisho matukufu ya Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu Nabii Adam AS, Nabii Ibrahim AS na Bwana wetu Muhammad SAW. Dua, kuomba maghufira, kunong'ona na Mwenyezi Mungu na kumshukuru Allah kwa neema Zake ni katika amali kubwa zinazofanyika kwenye ardhi ya Arafa. Hiyo ni fursa ya kipekee ambayo yumkini isirudi tena kwa mahujaji hao, na ni fursa bora ya kutubu madhambi yao toba ya kweli na kujiandaa kwa ajili ya amali za siku ya pili, siku ya Idul Adh'ha.

Mwezi tisa Mfunguo Tatu ni siku yenye sura na mazingira ya kipekee. Ijapokuwa sikukuu ya Idul Adh'ha ni siku ya kumi ya Mfunguo Tatu, lakini inaonekana kana kwamba upepo mwanana wa rehema za Mwenyezi Mungu huanza kupuliza katika siku ya kabla yake, siku ya Arafa. Dini tukufu ya Kiislamu umetilia mkazo mkubwa utukufu wa siku ya Arafa. Siku ya Arafa ni siku ya kudiriki na kuelewa maumbile ya Mwenyezi Mungu na neema Zake nyingi ambazo amewapa waja Wake. Arafa ni katika siku zenye utukufu wa kipekee na tumehimizwa mno kuitumia vizuri kwa ibada siku hiyo kadiri tunavyoweza. Sasa swali linalojitokeza hapa ni kwamba, ni vipi siku hiyo tukufu tunaweza kuitumia vizuri kadiri inavyowezekana?

Kufanya amali zote zinazomkurubisha zaidi mja kwa Mwenyezi Mungu kama vile kusoma Qur'ani sana, kufunga, kuomba dua, kukithirisha dhikri ni katika amali tunazohimizwa sana kuzifanya katika siku ya Arafa, yaani mwezi Tisa Mfunguo Tatu. Imam Sadiq AS, mmoja wa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akisema: Omba dua yoyote ile unayoipenda na hakikisha kuwa unakithirisha dua katika siku ya Arafa. Dua muhimu katika siku ya Arafa ni kuomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu kiasi kwamba suala hilo la istighfar na kuomba toba linaonekana kufunika ibada nyingine zote za siku ya Arafa.

Katika siku ya tisa ya Mfunguo Tatu kumeusiwa ibada nyingi na viongozi maasumu wa dini tukufu ya Kiislamu. Miongoni mwake kama tulivyoashiria hivi punde, ni kufunga, kukoga, kusali sala za suna na kuomba dua kwa wingi. Miongoni mwa tasbihi zilizokuwa zikisomwa na Bwana Mtume Muhammad SAW katika siku ya Arafa ni ile yenye maana isemayo: ...ametakasika Mwenyezi Mungu Ambaye Ndiye anayeudhibiti moto, ametakasika Mwenyezi Mungu Ambaye rehema Zake zimeenea katika pepo, ametakasika Mwenyezi Mungu Mtukufu Ambaye uadilifu Wake utadhihirika Siku ya Kiyama... Amma moja ya dua muhimu na ambayo imekusanya mambo mengi kwa ajili ya siku ya Arafa, ni dua ya Imam Husain AS, mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW aliyokuwa akiisoma kwenye jangwa la Arafa katika siku ya tisa ya Mfunguo Tatu. Dua hiyo imejaa maneno matukufu ya kuonesha utukufu na adhama isiyo na kifani ya Mwenyezi Mungu na udhaifu usio na kikomo wa mja mbele ya Muumba wake. Kumenukuliwa dua nyingine pia kutoka kwa Maimamu maasumu ambazo nazo zina umuhimu kuzisoma siku ya Arafa yaani siku ya tisa ya Mfunguo Tatu, Dhulhijja.

Ni jambo lisilo na shaka kwamba siku ya Arafa ina umuhimu mkubwa zaidi kwa watu ambao wako Makkah ambao wamepata bahati ya kwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hijja. Kwa hakika watu hao huanza amali yao ya Hija kwa kisimamo katika jangwa la Arafa. Mahujaji katika eneo hilo takatifu ambalo Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu kama vile Nabii Adam na Nabii Ibrahim AS pamoja na Mtume Muhammad, Bwana wa Mitume SAW  na kiumbe mtukufu zaidi kuliko viumbe wote wengine, wana kumbukumbu nyingi, walilitumia kwa ajili ya kuomba maghufira, kusoma dua na kumshukuru Muumba wao. Kuweko katika eneo hilo takatifu ni fursa ya kipekee ambayo si kila mtu hupata bahati ya kuwa na fursa hiyo, na wengi huipata mara moja tu katika umri wao wote. Imam Ali bin Abi Talib AS amenukuliwa akisema: Arafa ni eneo lililoko nje ya mipaka ya Haram na mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah wana wajibu wa kuonesha unyenyekevu wao kwenye eneo hilo kabla ya jambo lolote, ili wapate ustahiki wa kuingia kwenye Haram tukufu ya Mwenyezi Mungu. Vile vile amesema: Baadhi ya madhambi ya watu ni makubwa kiasi kwamba hayawezi kusamehewa katika eneo lolote ila kwenye jangwa la Arafa. Ndio maana, katika ardhi hiyo ya jangwani lakini iliyotakaswa na kupewa utukufu mkubwa na Mwenyezi Mungu, mahujaji huitumia fursa ya kuwepo hapo kuomba mno maghufira na msamaha wa Mola wao, ili watakasike kabla ya kupiga hodi na kuingia katika Haram tukufu huko Makkah, Haram ambayo Mwenyezi Mungu ameisifu katika Qur'ani kwa kusema, anayeingia humo yuko salama.

Vile vile imepokewa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW ambaye amesema: Wakati watu wanaposimama katika jangwa la Arafa, na kumuomba Mwenyezi Mungu kwa kulia na unyenyekevu mkubwa, Mwenyezi Mungu hujifakharisha mbele ya Malaika Wake kutokana na waja Wake hao na kuwaambia Malaika kwamba: Je, hamuoni waja Wangu wametoka maeneo ya mbali wakiwa wamejaa vumbi wamesimama kuniomba, na wametumia mali yao katika njia Yangu na miili yao imechoka? Ninaapa kwa utukufu na adhama Yangu, nimebadilisha madhambi yao kuwa mema kwao na nimewasafisha na madhambi na wamekuwa sawa na siku walipozaliwa na mama zao. Bwana Mtume Muhammad SAW amenukuliwa pia akisema: Mtu muovu zaidi siku ya Arafa ni yule ambaye ataondoka katika eneo hilo bila ya kusamewehewa madhambi yake

Arafa ni kivuko cha kuingilia katika eneo takatifu la Mina. Na sababu yake ni kuwa, mahujaji wanapopitisha siku tatu katika eneo hilo Mina, wanatakiwa kumpiga mawe mara tatu shetani na kila dhihirisho la shetani ili kujiweka mbali naye. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Siku ya Arafa ni muhimu sana kwa mahujaji. Mahujaji huhakikisha wanakuwa na utulivu mkubwa katika jangwa la Arafa, ili wapate fursa ya kumaliza kiu yao yote ya kunog’ona na kuomba toba na kuzitakasa nafsi pamoja na kujiweka mbali na ushawishi wa shetani.   

Mwaka jana pia, mahujaji kutoka kila kona ya dunia walitekeleza ibada za Arafa kwa shauku na kwa njia bora kabisa. Walitekeleza kwa ikhlasi na kwa unyofu wa hali ya juu. Baada ya kumaliza ibada za Arafa, mahujaji hao kama kawaida walielekea Mash'arul Haram kwa ajili ya kujiandaa kuelekea kwenye eneo la Mina bila ya kujua kuwa kuna janga zito mno linawasubiri huko Mina. Na hakukuwa na haja kwao ya kuwa na wasiwasi wowote kwani idadi ya mahujaji mwaka jana ilipungua mno ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma na kulihitajika umakini mdogo tu kuweza kusimamia ibada hiyo tukufu kwa njia bora kabisa. Hata hivyo maafa yanatarajiwa kutokea wakati wowote kwa utawala wa ukoo wa Aal Saud ambao umeshindwa hata kuendesha kwa njia sahihi nchi hiyo.

Kusimama Arafa katika jangwa lenye joto kali na baadaye kuelekea Mash'arul Haram kunawafanya mahujaji wachoke mno. Hivyo kitendo cha mahujaji cha kuelekea eneo la Mina asubuhi ya siku ya pili kwa ajili ya kumpiga mawe sheteni licha ya kuwa na uchofu mkubwa kupindukia, hakifanyiki ila kutokana na mapenzi makubwa sana wanayokuwa nayo mahujaji kwa Mola Muumba na imani thabiti kwa mafundisho ya dini yao. Wanafanya hivyo kwa sababu wana yakini na ahadi ya Mwenyezi Mungu waliyoipata katika jangwa la Arafa kwamba wamesamehewa madhambi yao na hivyo sasa umewadia wakati wa kumpiga mawe shetani na jeshi lake na kutangaza kujibari na kujiweka mbali nao. Lakini jambo la kusikitisha ni kuwa, maafisa waliokosa sifa ya kusimamia amali ya Hija wa Saudi Arabia walilielekeza wimbi kubwa la mahujaji katika kibarabara chembamba ambacho nacho kilikuwa kimefungwa pande zake zote mbili za asili, za kuingilia na kutokea. Licha ya hali kuwa hivyo, lakini mahujaji kutoka njia nyinginezo waliendelea kuruhusiwa kumiminika kwenye njia hiyo moja, iliyofungwa mbele na nyuma suala ambalo lilisababisha maafa makubwa ya kutisha yaliyopelekea maelfu ya mahujaji kuuawa kwa umati bila ya hatia wala sababu yoyote, kutokana na uzembe wa maafisa hao wanagenzi wa Saudia.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape malazi mema mahujaji wote waliouawa shahidi katika ibada ya Hija ya mwaka jana na awaingize katika kundi la watu waliotajwa na Mwenyezi Mungu aliposema katika aya ya 100 ya Suratun Nisaa kwamba:

وَمَنْ یَخْرُجْ مِنْ بَیْتِهِ مُهَاجِرًا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ یُدْرِکْهُ الْمَوْتُ فَقَدْ وَقَعَ أَجْرُهُ عَلَى اللَّهِ وَکَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِیمًا

...Na anayetoka nyumbani kwake kuhama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, kisha yakamfika mauti njiani basi umethibiti ujira wake kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.

3488737

Kishikizo: hija arafa
captcha