Katika mazungumzo yake hayo ya simu na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani, Rais Masoud Pezeshkian amehimiza kuimarishwa zaidi uhusiano pande mbili pamoja na kushirikiana katika kutatua migogoro ya Ghaza, Lebanon na Syria.
Amegusia pia vitendo vya kikatili vya magenge ya kigaidi huko kaskazini mwa Syria na kusisitiza kuwa, tunachotaka sisi ni kuishi katika eneo lenye usalama na linaloheshimiwa haki ya kujitawala kila shibri ya ardhi za nchi zote za eneo hili. Tunataka mataifa yote yaishi kwa usalama na utulivu na hilo haliwezekani isipokuwa kwa ushirikiano wa viongozi wa nchi za eneo hili na kutoruhusu madola baki ya kigeni kuingilia masuala ya ndani ya eneo hili.
Rais Pezeshkian amezungumzia pia nafasi muhimu sana ya Qatar katika upatanishi na utatuzi wa migogoro ya ukanda huu hususan kadhia ya Ghaza na ameishukuru Doha kwa hilo. Aidha amesema: Ni matumaini yetu nia na azma ya Qatar ya kuleta amani na utulivu katika eneo hili itaendelea kushuhudiwa kwenye masuala yote ili kwa njia hiyo tuweze kushirikiana zaidi, kuongeza nguvu na mshikamano wa nchi za Kiislamu na kuimarisha amani na usalama katika eneo letu hili.
Kwa upande wake Amir wa Qatar amesema kuwa, utulivu, usalama na amani nchini Syria haitoweza kupatikana isipokuwa kupitia mazungumzo na utatuzi wa kisiasa na kwamba Doha iko tayari kushiriki kikamilifu katika juhudi hizo.
3490915