IQNA

Iran yatoa wito kwa jamii ya kimataifa kusitisha mauaji ya kimbari Gaza

23:21 - April 28, 2025
Habari ID: 3480607
IQNA – Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito wa kuwepo harakati za jamii ya kimataifa ili kusitisha mauaji makubwa ya kimbari ya karne hii. 

Akizungumza kwa simu na mwenzake wa Saudi Arabia Jumapili usiku, Abbas Araghchi alifafanua msimamo wa Iran kuhusu matukio ya kikanda na kulaani ongezeko la ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi kutokana na uhalifu unaoendelea wa utawala wa Israeli katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, pamoja na mashambulizi yake ya mara kwa mara dhidi ya Lebanon. 

Amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za haraka kukomesha mauaji makubwa ya kimbari yanayoendelezwa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina w Gaza. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, Wapalestina wasiopungua 52,243 wameuawa katika vita vya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza tangu Oktoba 2023.

Araghchi pia alimfahamisha waziri wa Saudi kuhusu mwenendo wa hivi karibuni wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani. 

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al Saud, alieleza rambirambi zake kufuatia tukio la kusikitisha lililosababisha moto na mlipuko mbaya katika Bandari ya Shahid Rajaei kusini mwa Iran. 

Amewasilisha salamu za rambirambi na mshikamano kwa familia za waathiriwa, pamoja na serikali na watu wa Iran, akimuomba Mwenyezi Mungu awaponye majeruhi na kuwapa afya njema. 

Mawaziri hao wawili pia walijadili uhusiano wa pande mbili, pamoja na matukio ya kikanda na kimataifa wakati wa mazungumzo hayo ya simu.  

3492859

Habari zinazohusiana
captcha