Kwa mujibu wa Tume Kuu ya Uangalizi wa Masuala ya Msikiti Mtukufu wa Makkah na Msikiti wa Mtume (SAW), zaidi ya watu milioni 20 wamenufaika na huduma hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, vyombo vya habari vya Saudi vimeripoti Jumanne.
Huduma hizo ni pamoja na watu zaidi ya milioni 17 waliopatiwa miongozo ya mwelekeo (huduma za kuelekeza), zaidi ya milioni 3.28 waliotumia magari maalumu ya usaidizi wa kutembea, na zaidi ya 227,000 waliotumia huduma za kuhifadhi mizigo.
Zaidi ya mahujaji 525,000 walinufaika na huduma ya Tahallul, hatua ya ibada inayomaanisha kumalizika kwa sehemu au kwa jumla ya hali ya Ihram. Aidha, mamlaka hiyo iliripoti kugawa zaidi ya chupa milioni 3.66 za maji ya Zamzam na kuondoa zaidi ya tani 9,700 za taka ili kudumisha usafi ndani na kuzunguka Msikiti.
Katika hatua nyingine inayohusiana, Urais wa Masuala ya Kidini umeanzisha mpango mpya wa kuwasaidia mahujaji wa Umrah kwa msimu wa mwaka 1447 Hijria. Mpango huo unahusisha usambazaji wa nakala za Qur’an Tukufu, vijitabu vya elimu ya ibada, na zawadi kwa mahujaji.
Maafisa wamesema lengo ni kutoa huduma za kina za mwongozo ili kuwasaidia mahujaji kuelewa vizuri na kutekeleza ibada zao kwa ufanisi, pamoja na kueneza mafunzo na thamani za kiroho zinazohusiana na Misikiti Miwili Mitukufu.
Msikiti Mtukufu wa Makkah, au Al-Masjid al-Haram, ni mahala patakatifu zaidi katika Uislamu na ndio kitovu cha ibada ya Hajj inayofanyika kila mwaka pamoja na ibada ya Umrah inayofanyika mwaka mzima. Mamilioni ya Waislamu kutoka kila pembe ya dunia husafiri kuelekea Makkah kwa ajili ya kutekeleza ibada hizi tukufu.
3493761