Kwa mujibu wa Waziri wa Masuala ya Kidini wa Malaysia, Mohammad Na’im Mokhtar, jumla ya washiriki 72 kutoka nchi 50 watashiriki katika mashindano ya mwaka huu. Kati ya hao, 40 watashindana katika kipengele cha usomaji wa Qur’ani, huku 32 wakishiriki katika kipengele cha kuhifadhi Qur’ani.
"Zoezi la kuchuja washiriki lilifanyika kwa njia ya mtandaoni kuanzia Mei 19 hadi 23, na lilifanywa na jopo la majaji waliobobea ili kuhakikisha haki na uwazi," alisema waziri huyo wakati wa hafla ya utangulizi wa mashindano hayo jijini Kuala Lumpur siku ya Jumatatu.
Mashindano ya mwaka huu yanabeba kaulimbiu "Kuijenga Ummah wa MADANI", na yatazinduliwa rasmi na Waziri Mkuu Anwar Ibrahim tarehe 2 Agosti.
Malaysia itawakilishwa na Aiman Ridhwan Mohamad Ramlan (kutoka Perak) na Wan Sofea Aini Wan Mohd Zahidi (kutoka Terengganu) katika kipengele cha usomaji wa Qur’ani, pamoja na Muhammad Adib Ahmad Rozaini (Perak) na Putri Auni Khadijah Mohd Hanif (Kelantan) katika kipengele cha kuhifadhi.
Kwa mujibu wa Mohd Na’im, jopo la majaji kwa mwaka huu linajumuisha wataalamu 16 kutoka nchi mbalimbali kama vile Malaysia, Saudi Arabia, Misri, Jordan, na Indonesia; hii ikiwa ni kuhakikisha mchakato wa upimaji unazingatia viwango vya kitaalamu na haki kwa wote.
Alieleza kuwa kipengele cha usomaji kitapimwa kwa kuzingatia vipengele vinne: tajwīd (usahihi wa matamshi), tarannum (mbinu ya kusoma kwa lahani), fasaha (ustadi wa lugha) na ubora wa sauti. Kipengele cha kuhifadhi kitapimwa kwa usahihi wa hifadhi na mtiririko sahihi wa usomaji.
Akizungumzia uteuzi wa kaulimbiu, Mohammad Na’im alisema inalingana na dira ya Malaysia ya kukuza jamii iliyoendelea, si tu kwa maendeleo ya miundombinu bali pia kwa ukuaji wa kiroho, kielimu na kimaadili.
Aliongeza kuwa Malaysia imetambulika kwa muda mrefu kama mwenyeji bora wa mashindano ya MTHQA tangu kuanzishwa kwake tarehe 8 Machi, 1961, na mojawapo ya mafanikio yake ni kupokea Tuzo ya Mpango Bora wa Qur’ani kutoka Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani ya Kuwait mwaka 2016.
“JAKIM itaendelea kuinua hadhi na ubora wa tukio hili, sambamba na mahitaji ya sasa ikiwa ni pamoja na ujumuishaji wa teknolojia za kidijitali na akili mnemba (AI),” aliongeza waziri huyo.
Washindi wa kwanza katika kila kipengele watapokea zawadi ya pesa taslimu RM40,000, wa pili RM30,000, na wa tatu RM20,000, pamoja na zawadi za vito kutoka kwa Shirika la Maendeleo ya Uchumi wa Kiislamu Malaysia (YaPEIM).
Kama sehemu ya mashindano haya, tukio maalum la usomaji wa Qur’ani kutoka KL Sentral hadi Hatyai litaandaliwa, likiwa na lengo la kuweka rekodi mpya katika Kitabu cha Rekodi cha Malaysia (Malaysia Book of Records) kwa kipengele cha "Usomaji wa Qur’ani Mrefu Zaidi Katika Safari ya Treni ya Kimataifa ya Mpaka."
3493845