Qari kutoka Malaysia, Aiman Ridhwan Mohamad Ramlan, na qariah Wan Sofea Aini Wan Mohd Zahidi wote wawili walishinda nafasi ya kwanza katika kipengele cha kisomo (tilawa). Tuzo zao walikabidhiwa katika hafla ya kufunga mashindano hayo yaliyofanyika jijini Kuala Lumpur siku ya Jumamosi, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Malaysia.
Aiman Ridhwan alipata alama za juu zaidi kwa asilimia 97.01, akiwashinda Ahmad Azroi Hasibuan kutoka Indonesia (asilimia 95.13) na Muhammed Yahya Yildizhan kutoka Uturuki (asilimia 93.88) waliomaliza nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.
Katika kipengele cha wanawake, Wan Sofea Aini alipata asilimia 95.88, akimzidi Fatima Zahra Assafar wa Morocco (asilimia 89.38) na Nur Rahmiyatin Adhya wa Indonesia (asilimia 87.59).
Katika kipengele cha wanawake cha kuhifadhi Qur’ani Tukufu (hifdhi), Putri Auni Khadijah Mohd Hanif wa Malaysia alipata nafasi ya pili kwa asilimia 96.75, huku ubingwa ukichukuliwa na Tasneem Arian Omar wa Syria aliyepata asilimia 97.5.
Kwa upande wa wanaume katika kipengele cha hifdhi, Usamah Barghouth kutoka Ujerumani alitwaa ubingwa kwa asilimia 98.25, akifuatwa na Mohammad Abdullah Masasati wa Syria (asilimia 98.01) na Mohammad Jamil Farhat wa India (asilimia 97.25).
Hafla ya kutoa zawadi ilihudhuriwa na Waziri Mkuu Anwar Ibrahim, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Masuala ya Kidini) Datuk Mohd Na’im Mokhtar, pamoja na Spika wa Bunge la Wawakilishi Tan Sri Johari Abdul.
3494182