Katika ujumbe wake aliotoa siku ya Alkhamisi, Kiongozi Muadhamu amesema Iran iliuponda utawala wa Kizayuni wa Israel na kuupigisha magoti na kuionesha Marekani kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaweza kufikia vituo muhimu vya Marekani katika eneo na kuchukua hatua dhidi yao.
Ifuatayo ni matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu
Salamu kwa taifa kubwa na pendwa la Iran.
Kwanza, ninaenzi kumbukumbu ya mashahidi wenye hadhi wa matukio ya hivi karibuni wakiwemo makamanda na wanasayansi waliouawa kishahidi ambao walikuwa wa thamani sana kwa Jamhuri ya Kiislamu na waliitumikia kwa uaminifu. Leo, wanapokea thawabu kwa ajili ya utumishi wao bora mbele ya Mwenyezi Mungu, Inshallah.
Ninaona ni muhimu kulipongeza taifa kubwa la Iran. Ninatoa pongezi kadhaa:
Kwanza pongezi kwa ushindi dhidi ya utawala bandia wa Kizayuni.
Utawala wa Kizayuni kwa kelele na majigambo yake yote ulikandamizwa na kupigishwa magoti kufuatia mapigo ya Jamhuri ya Kiislamu. Wazo kwamba mapigo kama hayo yangeweza kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu halikuwahi hata kuingia akilini mwao—lakini ilitokea. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulisaidia Jeshi letu, kwa kuwawezesha wanajeshi kupenya mifumo yao ya juu ya ulinzi yenye tabaka nyingi na kubomoa kikamilifu maeneo mengi ya mijini na kijeshi kwa mashambulizi makali ya makombora na silaha za hali ya juu. Hii ni moja ya baraka kuu za Mwenyezi Mungu. Inathibitisha kwamba utawala wa Kizayuni lazima uelewe kwamba uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unakuja kwa gharama kubwa—gharama kubwa sana. Kwa neema ya Mwenyezi Mungu, hili lilifanyika, na sifa iende kwa Jeshi letu na wananchi wetu wapendwa, ambao walilea, kufundisha, na kuunga mkono vikosi hivi, wakiimarisha uwezo wa kutimiza kazi kubwa kama hiyo.
Pongezi za pili kwa ushindi wa Iran dhidi ya utawala wa Marekani.
Utawala wa Marekani uliingia katika mapambano ya moja kwa moja kwa sababu ulitambua kwamba bila ya kuingilia, utawala wa Kizayuni ungeangamizwa kabisa. Waliingilia kati ili kuokoa utawala huo lakini hawakupata chochote kutokana na vita hivi. Walishambulia vituo vyetu vya nyuklia lakini hawakufanikiwa kwa lolote muhimu. Hujuma hiyo inaweza kufuatiliwa na kulalamikiwa kisheria katika mahakama za kimataifa. Rais wa Marekani alitumia madai ya kutia chumvi katika kuelezea yaliyojiri katika mashambulizi hayo. Ni wazi alihitaji kutia chumvi. Yeyote aliyesikiliza angeweza kuona kwamba maneno yake yalificha ukweli, walishindwa katika malengo yao na waliamua kutia chumvi ili kuficha ukweli. Hapa pia, Jamhuri ya Kiislamu iliibuka mshindi, ikilipiza kisasi kwa kofi kali kwa uso wa Marekan, kwa kupiga moja ya vituo vyake muhimu vya kikanda, Al-Udeid, na kusababisha uharibifu. Wale wenye kukuza mambo walijaribu kudunisha pigo, wakidai "hakuna kilichotokea", wakati kwa kweli tukio kubwa lilikuwa limetokea. Ukweli kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaweza kufikia ngome muhimu za Marekani katika eneo na kuchukua hatua dhidi yao ipendavyo si jambo dogo—ni jambo muhimu, na linaweza kurudiwa katika siku zijazo. Uchokozi wowote wa siku zijazo utakuja kwa gharama kubwa kwa adui.
Tatu pongezi kwa umoja wa ajabu wa taifa la Iran.
Kwa neema ya Mungu, taifa la karibu watu milioni 90 lilisimama kwa umoja, bega kwa bega, bila mgawanyiko wowote wa mahitaji au malengo. Walipaza sauti zao na kutangaza kuunga mkono hatua za Wanajeshi—na hili litaendelea. Taifa la Iran lilidhihirisha adhama yake, sifa zake mashuhuri, na kuthibitisha kwamba wakati wa lazima, taifa hili huzungumza kwa sauti moja. Na kwa neema ya Mungu, hii ilifanyika.
Jambo muhimu ambalo nataka kusisitiza ni kwamba rais wa Marekani hivi karibuni alisema Iran lazima ijisalimishe. Jisalimishe! Hili halihusu tena urutubishaji urani, tasnia ya nyuklia, au kisingizio kingine chochote-ni kuhusu kujisalimisha kwa Iran. Bila shaka, maneno kama hayo ni makubwa sana kwa kinywa cha rais wa Marekani. Kwa kuzingatia adhama ya Iran, pamoja na historia yake, utamaduni, na azimio la kitaifa lisiloweza kusambaratishwa-wazo la kutaka kujisalimisha kwa nchi kama hiyo ni la kichekesho kwa wale wanaojua taifa la Irani. Lakini kauli yake ilifichua ukweli: Tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani imekuwa katika mzozo na Iran ya Kiislamu, siku zote ikipata visingizio vipya—haki za binadamu, demokrasia, haki za wanawake, urutibishaji, suala la nyuklia, uundaji wa makombora—lakini suala la msingi ni jambo moja tu kujisalimisha kwa Iran. Viongozi wa awali wa Marekani hawakusema moja kwa moja kwa sababu haikubaliki-hakuna mantiki ya inayokubali kuliambia taifa, "Njoo, jisalimishe". Kwa hivyo waliificha nia yao nyuma ya kauli zingine. Lakini mtu huyu alifichua ukweli: Marekani haitakubali chochote zaidi ya kujisalimisha kwa Iran. Hili ni jambo muhimu! Taifa la Iran lazima lijue kwamba huu ndio mzizi wa mzozo na Marekani—tusi kubwa hili kwa Iran—na jambo kama hilo halitatokea kamwe. Kamwe.
Taifa la Iran ni taifa kubwa. Iran ni nchi yenye nguvu na kubwa yenye ustaarabu wa kale. Utajiri wetu wa kitamaduni na kiustaarabu ni mkubwa mara mia kuliko ule wa Marekani na inayoipenda. Kutarajia Iran itajisalimisha kwa nchi nyingine ni hadaa ya kipuuzi ambayo inaweza kupelekea mwenye matarajio hayo kujejeliwa na watu wenye hekima na maarifa. Taifa la Iran ni lenye heshima na litaendelea kuwa hivyo, lenye ushindi na ni ushindi kwa neema ya Mwenyezi Mungu. Tunaomba kwamba Mwenyezi Mungu daima alihifadhi taifa hili chini ya baraka Zake kwa utu na heshima, anyanyue hadhi ya Imamu mkuu [Khomeini], na iwepo ridhaa ya Imam Mahdi (roho zetu zitolewe mhanga kwa ajili yake), ili uungaji mkono wake ubaki kwa umma huu.
Wa Asalamu Alaikum wa Rahmatullah wa Barakatuh
4291001