Barua hiyo, iliyoratibiwa na shirika la misaada kwa wakimbizi, Choose Love, inaitaka serikali ya Uingereza kusitisha mara moja usafirishaji wa silaha kwa Israel, kufungua njia za misaada ya kibinadamu bila vikwazo, na kuhimiza kusitisha mapigano ili kuokoa maisha ya Wapalestina.
Miongoni mwa walioandika barua hiyo ni Dua Lipa, Gary Lineker, Benedict Cumberbatch, na wanamuziki kama Annie Lennox na wanachama wa Massive Attack. Pia, manusura wa mauaji ya Holocaust, Stephen Kapos, ameungana nao katika kutoa wito huo.
Barua hiyo inaishtumu serikali ya Uingereza kwa kusaidia kampeni ya kijeshi ya Israel kwa kusambaza vipengele vya silaha vinavyotumika katika mashambulizi ya anga, na kutofanya lolote licha ya ushahidi wa mauaji ya kimbari Inatoa taswira ya janga la kibinadamu linaloshuhudiwa Gaza, ambako maelfu ya watoto wanakabiliwa na utapiamlo mkali kutokana na vizuizi vya Israel vya chakula na dawa.
Aidha, shinikizo linaongezeka kutoka kwa wataalamu wa sheria, waandishi wa habari, na wanaharakati wa haki za binadamu. Wanasheria wa Uingereza wameonya kuwa uendelezaji wa ushirikiano wa kijeshi na Israel unaweza kuifanya Uingereza kuwa mshirika wa uhalifu wa mauaji ya kimbari. Waandishi mashuhuri, akiwemo Zadie Smith na Ian McEwan, wameandika barua ya wazi wakitaka usitishaji wa mapigano na usambazaji wa misaada bila masharti.
Tangu Oktoba 2023, zaidi ya Wapalestina 54,000, wakiwemo watoto 15,000, wameuawa katika mashambulizi yanayoendelezwa na utwala haramu wa Israel. Nusu milioni wanakabiliwa na hatari ya njaa kali. Sasa, sauti za upinzani kutoka kwa wasanii, wanasheria, na wanaharakati zinaongeza shinikizo kwa Uingereza kuchukua hatua dhidi ya uhalifu wa kivita unaoendelea Gaza.
3493273/