IQNA

Gavana wa Misri asema marehemu Qari Shuaisha alikuwa balozi bora wa Qur’ani

15:11 - August 19, 2025
Habari ID: 3481105
IQNA – Gavana wa mkoa wa Kafr el-Sheikh nchini Misri amesema kuwa marehemu qari Sheikh Abulainain Shuaisha alikuwa balozi bora wa Qur’ani na ataendelea kubaki kuwa fahari ya Misri.

Alaa Abdel Mu’ti, kupitia ujumbe wake wa kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa qari huyo mashuhuri kwa mara ya 103, alisema kuwa Sheikh Shuaisha alikuwa chanzo cha heshima kwa Misri wakati wa uhai wake na bado anaendelea kuwa chanzo cha fahari ya taifa, gazeti la Al-Watan liliripoti.

Alisema kuwa Sheikh Shuaisha ni miongoni mwa alama za usomaji wa Qur’ani ambazo zitaendelea kudumu milele katika historia.

Kwa mujibu wa Abdel Mu’ti, Sheikh Shuaisha hakuwa msomaji tu wa Qur’ani, bali alikuwa ni “chuo cha usomaji” chenyewe, ambapo sauti yake ya kipekee na unyenyekevu katika usomaji vilijikita mioyoni mwa Waislamu kote duniani.

Alisisitiza kuwa Sheikh Shuaisha hakuwa wa Misri pekee, bali alisafiri katika nchi nyingi duniani akiibeba Misri na Uislamu, na kwa kusambaza maneno ya Mwenyezi Mungu kupitia sauti yake ya kupendeza, alikuwa balozi bora kabisa wa Qur’ani.

Akitaja kuwa Sheikh Shuaisha alitoka mkoani Kafr el-Sheikh, gavana alibainisha kuwa hilo ni jambo la heshima kubwa kwa mkoa huo na akawataka vizazi vipya waige mfano wa qari huyu maarufu wa Kimasri.

Sheikh Abulainain Shuaisha alizaliwa Agosti 22, 1922, na maisha yake yote alitumia kufufua mitindo halisi ya usomaji wa Qur’ani. Ameelezewa kuwa ni miongoni mwa majina makubwa yasiyosahaulika katika historia ya usomaji, akijulikana kwa sauti yake yenye nguvu iliyofanana na chuma.

Alianza kusoma Qur’ani akiwa na umri mdogo na kujiunga na majukwaa ya usomaji yaliyohudhuriwa na makari mashuhuri. Wengine wamemwona kama mhimili usioweza kurudiwa tena katika nyanja ya usomaji wa Qur’ani.
Sauti yake ya kipekee, iliyoitwa “sauti ya chuma,” ilikuwa imara, yenye msisitizo na inayotia msisimko.

Qari wengi wamejaribu kuiga mtindo wa usomaji wa Sheikh Shuaisha lakini hakuna aliyeweza kufikia upekee wake, kwani sauti na mbinu yake vilikuwa vya kipekee na vigumu kuiga.

Pamoja na Sheikh Abdul Basit Abdul Samad, alianzisha Jumuiya ya Waqari wa Qur’ani ya Misri, na mwaka 1988 alichaguliwa kuwa rais wa jumuiya hiyo.

Sheikh Shuaisha alisafiri nchi nyingi kwa ajili ya kusoma Qur’ani na aliheshimiwa kwa usomaji wake bora nchini Lebanon, Syria, Iraq, Uturuki, na Jordan miongoni mwa zingine.
Alikuwa qari wa kwanza wa Kimasri kusoma Qur’ani katika Msikiti wa Al-Aqsa ulioko katika mji mtakatifu wa Quds (Jerusalemu).

Aidha, alisafiri mara kadhaa nchini Iran na kuhudumu kama mmoja wa majaji katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ya Qur’ani nchini humo.

Qari huyu maarufu alifariki Juni 23, 2011, akiwa na umri wa miaka 89, baada ya kuugua kwa miezi mitatu.

3494297

Habari zinazohusiana
Kishikizo: shuaisha qari misri
captcha