
Kituo cha Nasyrul Qur’an, ambacho ni cha pili kwa ukubwa duniani katika uchapishaji wa Qur’an, kinachapisha tafsiri au tarjuma hizi kama sehemu ya mradi wa One Million Qur’an Waqf Solidarity.
Uzinduzi wa uchapishaji huo ulifanywa na Naibu Waziri wa Kazi, Ahmad Maslan, pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Restu, Abdul Latif Mirasa, na Rais wa Shirika la Misaada ya Kibinadamu na Uokoaji la Malaysia (MAHAR), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ops Ihsan, Jismi Johari.
Katika taarifa yake, Nasyrul Qur’an pia ilitangaza kuwa nakala 20,000 za Qur’an za waqf ziko tayari kusambazwa huko Zanzibar nchini Tanzania, ili kuunga mkono elimu ya Kiislamu na kuwawezesha Waislamu wa eneo hilo, ambao wanahitaji kwa dharura nakala za Qur’an zenye ubora wa juu.
Aidha, kwa msaada wa baada ya majanga nchini Malaysia, Aceh na Thailand Kusini, jumla ya nakala 10,000 za Qur’an za waqf zimetengwa ili kuchukua nafasi ya nakala zilizoharibiwa na majanga ya kiasili.
Akizungumza, Ahmad alisema juhudi hii si shughuli ya uchapishaji pekee bali ni jukumu la da‘wah linalovuka mipaka ya kijiografia.
“Kupitia mpango wa One Million Qur’an, tunataka kuhakikisha hakuna Mwislamu anayebaki bila Qur’an anayoielewa. Uchapishaji wa nakala 20,000 za Qur’an zenye tafsiri ya Kitamil ni hatua ya kimkakati kufikia mamilioni ya wasemaji wa Kitamil, huku usambazaji wa Qur’an Zanzibar na maeneo yaliyoathirika na mafuriko ukionesha mshikamano wa Waislamu wa Malaysia na Waislamu wenzao nje ya nchi,” alisema.
Mradi wa One Million Qur’an Waqf Solidarity, uliochochewa na Waziri Mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim, unalenga kusambaza nakala za Qur’an zenye tafsiri katika lugha mbalimbali duniani kote.
3495791