IQNA

Washiriki wa Vikao vya Qur’ani Kosovo Waenziwa

14:13 - January 29, 2026
Habari ID: 3481866
IQNA – Hafla maalumu ilifanyika katika Msikiti wa Barduşit mjini Pristina, mji mkuu wa Kosovo, kwa lengo la kuwaenzi wanafunzi 80 wa kike wa Qur’ani walioshiriki katika duru za masomo ya Qur’ani Tukufu.

Katika hatua inayoonesha mafanikio ya programu za elimu ya dini kwa wasichana misikitini, Msikiti wa Barduşit uliandaa hafla hiyo ya kuwapongeza zaidi ya wanafunzi 80 wa kike waliokuwa wamejiandikisha katika duru za Qur’ani. Hafla hiyo ilikuwa sehemu ya juhudi za Idara ya Wanawake ya Kiislamu ya Kosovo katika kuendeleza elimu ya Kiislamu na kuwaunganisha vijana, hasa wasichana, na Qur’ani Tukufu.

Programu hiyo ilifanyika kwa lengo la kuunga mkono shughuli za kielimu za wasichana ndani ya misikiti, na ikawa ni jukwaa la kiroho la kuwahamasisha wanafunzi wa kike wa Qur’ani kuendelea katika njia ya hifdh na tilawa, wakipiga hatua kutoka ngazi za mwanzo za elimu hadi hatua za juu za usomaji na kuhifadhi Qur’ani.

Katika hafla hiyo, nakala za Qur’ani Tukufu ziligawiwa kwa wanafunzi saba wa kike waliokuwa wamekamilisha hatua ya kujifunza herufi za Kiarabu (hijaaiyya) na kuanza rasmi hatua ya usomaji wa Qur’ani. Aidha, zawadi ziligawiwa kwa washiriki wa duru za hifdh na kwa wale waliokuwa tayari wamehifadhi juzuu kadhaa za Qur’ani, kwa lengo la kuimarisha roho ya ushindani chanya, na kujenga haiba zilizo na mizani, zenye uelewa wa mwenendo na maadili ya Kiislamu.

Programu za aina hii zinaonesha wazi kuwa shughuli za kielimu katika misikiti ya Kosovo hazijikiti tu katika masomo ya darasani, bali ni programu jumuishi zinazolenga kujenga motisha, malezi ya tabia njema, na kuwapatia wasichana mazingira salama ya kujifunza na kuendelea chini ya usimamizi wa mfumo wa elimu uliopangiliwa na wenye dira ya Kiislamu.

Habari inayohusiana:

Kosovo, inayojulikana rasmi kama Jamhuri ya Kosovo, ni nchi isiyo na mwambao wa bahari iliyopo Kusini-Mashariki mwa Ulaya. Inapakana na Albania upande wa kusini-magharibi, Montenegro upande wa magharibi, Serbia upande wa kaskazini na mashariki, na Masedonia ya Kaskazini upande wa kusini-mashariki.

Leo hii, asilimia 95.6 ya wakazi wa Kosovo ni Waislamu, na wengi wao ni wa kabila la Waalbania. Aidha, wapo pia Waislamu wasiozungumza Kialbania, wanaojitambulisha kama Bosniak, Gorani, na Waturuki, ambao nao ni sehemu ya jamii ya Kiislamu ya Kosovo.

4330872

Kishikizo: kosovo qurani tukufu
captcha