
Aidha amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasalimu amri mbele ya tamaa na mashinikizo yasiyo ya haki ya Marekani, wala haitanyamaza mbele ya dhuluma na uvamizi. Hata hivyo, amesema Iran, kwa nguvu zake zote, inaendelea kujitolea kwa ajili ya amani na utulivu wa eneo.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amehutubia umma leo asubuhi katika hafla ya maadhimisho ya miaka arobaini na saba tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na maandamano makubwa ya tarehe 22 Bahman. Katika hotuba yake katika uwanja wa Medani ya Azadi jijini Tehran, awali alitoa salamu za heshima kwa roho tukufu ya muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu), na pia amewakumbuka mashahidi kwa taadhima, akaomba maisha marefu kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na akalipongeza taifa kwa sikukuu ya ushindi wa Mapinduzi.
Leo, Jumatano, Februari 11 mwaka 2026 inasadifian na tarehe 22 mwezi Bahman mwaka 1404 Hijria Shamsia kwa mujibu wa kalenda ya Iran ambayo ni siku ya maadhimisho ya kutimia mwaka wa 47 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Siku hii pia ni maarufu kama Yaumullah au Siku ya Mwenyezi Mungu kutokana na kujiri Mapinduzi ya Kiislamu katika siku hii.
Rais alisema kuwa dunia ya leo inapaswa kushuhudia namna ambavyo watu wa Iran, kwa mamilioni yao, walivyojitokeza kwa safu zilizojaa katika miji na maeneo mbalimbali ya nchi ili kuthibitisha uaminifu wao kwa uongozi, kulinda misingi ya Mapinduzi, na kutetea heshima, ardhi, na urithi wa taifa lenye historia na fahari ya Iran.
Rais Pezeshkian amesema kwamba Februari 11 ni "siku ambayo watu walisimama dhidi ya dhuluma, ukandamizaji, na uonevu."
Rais Pezeshkian ameashiria malengo ya harakati za mwamko wa taifa la Iran mwaka 1979, na kusema: "Wananchi wa Iran walifanya mapambano ili kusimamisha uadilifu na kuifanya Iran kuwa huru, na waliwadhihirishia walimwengu kwamba Wairani na Waislamu wana uwezo wa kujenga nchi yao kwa nguvu zao, irada, elimu na sanaa zao, na kujijengea heshima na uhuru wao."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria namna adui alivyojaribu kusambaratisha mapinduzi machanga ya nchi hii tangu siku ya kwanza ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamuu kwa hatua kama za kuibua migawanyiko na kufanya mapinduzi na kusema: "Marekani na Ulaya zilifanya njama zao zote ili kusambaratisha Mapinduzi yetu lakini ziligonga mwamba. Walitulazimisha vita vya miaka minane. Walimuunga mkono dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein ili kuigawa vipande na kuishinda Iran, hata hivyo vijana wetu walipambana na kuihami nchi, mfumo na Mapinduzi ya Kiislamu kwa ujasiri kwa kusabilia maisha yao."
Akiendelea na hotuba yake katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais wa Iran amesema: "Hii leo kama mashahidi wetu wangekuwepo tusingekabiliwa na matatizo mengi. Hawakutafuta dunia, ubinafsi, madaraka na umaarufu. Mashahidi wote hawa kuanzia Meja Jenerali Baqeri na Meja Jenerali Salami hadi Shahidi Soleimani, wote walisabilia maisha yao bila kujulikana kwa ajili ya nchi hii na Mapinduzi ya Kiislamu."
Habari inayohusiana:
Rais Pezeshkian amesisitiza umuhimu wa kuendezwa umoja na mshikamano wa ndani, na kwamba licha ya vitisho na njama za kutaka kupotosha vijana wa taifa, hakuna njia mbadala ila mshikamano.
"Sasa zaidi ya hapo awali, tunahitaji mwongozo wa busara wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ili kuweka kando matatizo na migawanyiko, kukurubisha pamoja mitazamo tofauti na kuongoza taifa kuelekea kwenye lengo lililo wazi," amesisitizia Rais Pezeshkian na kusema: Uwepo wa Kiongozi Muadhamu ni nguvu ambayo imeruhusu mfumo na Mapinduzi ya Kiislamu kusonga mbele kwa nguvu licha ya changamoto zote.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwenye Uwanja wa Azadi mjini Tehran, Pezeshkian ameangazia nafasi muhimu ya nchi za kikanda na za Kiislamu katika kuzuia njama za maadui. Amesema "nchi katika eneo hili, moja baada ya nyingine, zinashiriki wasiwasi na misimamo yao nasi kupitia mazungumzo."
4333629