
Waislamu wa eneo la Quiapo jijini Manila wana tamanio la kipekee wanapotekeleza ibada za Ramadhani mwaka huu: kujengwa kwa msikiti mpya katikati ya mji mkuu wa Ufilipino.
Shirika moja limewasilisha ombi kwa maafisa wakuu wa serikali ya Ufilipino, wakiwemo wabunge Waislamu katika Bunge la nchi hiyo, kuidhinisha ujenzi wa msikiti mpya katika sehemu ya Hifadhi ya Rizal, maarufu pia kama Luneta.
Kwa mujibu wa Markazuz Zakah, msikiti unaopendekezwa utakuwa mbadala wa Msikiti ulioharibiwa na majeshi ya Kihispania walipoivamia Manila katika miaka ya 1570.
“Kabla ya kuwasili kwa wakoloni Wahispania, Manila iliongozwa na Marajaa Waislamu, jambo linalothibitisha kuwa Uislamu ulikuwapo katika historia ya taifa letu muda mrefu kabla ya ujio wa Ukristo,” shirika hilo lilisema katika ombi lake.
“Zaidi ya hayo, msikiti katika eneo la Luneta utakuwa rasilimali muhimu kwa jamii ya Kiislamu. Utawapatia mahali pa kuswali, kujifunza dini yao, na kuimarisha mshikamano wao,” ombi hilo liliongeza.
Eneo la Rizal, lenye ukubwa wa hekta 58, liko katikati ya Manila, karibu na mji wa kale wa Kihispania wa Intramuros, ambao hapo awali ulikuwa eneo la ngome ya Rajah Sulayman, mtawala wa mwisho wa asili kabla ya uvamizi wa Ulaya.
Ndani ya eneo linalotazamana na Kanisa Kuu la Manila, wanahistoria wa Kiislamu wanaamini ndipo palipokuwapo msikiti wakati wa utawala wa Rajah Sulayman.
Eeno hilo limepewa jina la shujaa maarufu wa taifa la Ufilipino, José Rizal, ambaye kunyongwa kwake na utawala wa kikoloni wa Kihispania mnamo Desemba 1896 kulichochea mapinduzi ya kitaifa yaliyomaliza utawala wa Ulaya.
Leo, eneo la Rizal huwa mwenyeji wa maadhimisho ya kila mwaka ya Siku ya Uhuru, pamoja na matukio mbalimbali ya umma, yakiwemo misa za Kikatoliki na mikutano ya maandamano.
Historia ya Waislamu
Ufilipino ina takribani Waislamu milioni saba, wengi wao wakiishi katika Kisiwa cha Mindanao kusini mwa nchi, katika taifa lenye jumla ya wananchi wapatao milioni 115.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa kuenzi historia ya Kiislamu nchini humo, Rais wa Markazuz Zakah, Gambae Macatanong, alisema kuwa msikiti katika eneo muhimu zaidi la umma nchini Ufilipino ungekuwa ishara ya kutambua na kuheshimu urithi na historia tajiri ya Waislamu.
“Tunaomba kwa heshima uungwaji mkono kwa ujumbe huu wenye nguvu wa ujumuishi na utambuzi, kwa jamii ya Waislamu na taifa zima,” Macatanong alisisitiza.
Markazuz Zakah ilituma maombi yake kwa wabunge Waislamu Seneta Robinhood Padilla na Mwakilishi Haima Kiram Ismula, pamoja na Meya wa Manila Francisco Domagoso, na Katibu wa Utalii Ma. Esperanza Frasco.
Hadi sasa, hakuna hata mmoja kati ya walengwa wa maombi hayo aliyetoa majibu rasmi. Waombaji wamesema wanatumaini kusikia majibu hivi karibuni, hususan kutoka kwa viongozi wenzao Waislamu, kuhusu pendekezo hilo.
3496557