
Ustadh Hamed Shakernajad ameliambia Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) katika mahojiano kuwa Mahfel imeifanya Qur’ani kuwa msingi wa miradi na juhudi mbalimbali za kitamaduni kote Iran, na pia kimeisaidia kuitambulisha kizazi cha vijana uzuri wa Neno la Mwenyezi Mungu kwa lugha inayowakaribia na kuwafikia.
Kipindi cha Mahfel, kinachojulikana kwa kuonesha visomo vya Qur’ani na kukuza mafundisho ya Kiislamu, kinoheshimika na kupendwa na watazamaji katika sehemu mbalimbali za dunia.
Hutangazwa kupitia kituo cha cheneli ya IRIB TV3 kila siku takribani saa moja kabla ya adhana ya Magharibi katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, kikitoa mazingira ya kiroho kwa watazamaji wanapojitayarisha kufuturu.
Kikiwa na mkazo mkubwa juu ya Qur’ani Tukufu, kipindi hiki kinalenga kuyapa thamani na manufaa yale mapumziko mafupi ya wenye kufunga kwa mijadala yenye busara na visomo vya Qur’ani vinavyogusa nyoyo.
Ustadh Shakernajad, ambaye ni msomaji wa Qur’ani anayetambulika kimataifa na mmoja wa wahusika wakuu wa programu ya Mahfel, alizungumza na IQNA kuhusu mabadiliko ya mtazamo wa watu juu ya Qur’ani, athari za kijamii za programu hiyo, umuhimu wa kuishi na Qur’ani kwa vitendo, pamoja na wajibu wa kizazi cha leo katika kulea vijana wanaoishi kwa maadili ya Qur’ani.
Hapa chini ni baadhi ya dondoo kutoka katika mahojiano hayo:
IQNA: Bwana Shakernajad, ungeelezaje mazingira ya msimu wa nne wa Mahfel?
Shakernajad: Natoa salamu kwa watazamaji na wasomaji wote wa IQNA. Msimu wa nne wa Mahfel, kama ilivyokuwa katika misimu iliyotangulia, umejaa uhai na roho ya Qur’ani. Katika kipindi hiki tumekuwa tukijitahidi kuwasilisha kwa hadhira furaha na utamu wa kuishi pamoja na Qur’ani. Kila msimu mpya unaakisi namna jamii inavyozidi kuimarisha uhusiano wake na Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
IQNA: Wapo wanaoamini kuwa Mahfel si kipindi cha televisheni tu, bali imekuwa harakati ya kitamaduni. Wewe unaonaje?
Shakernajad: Ni kweli kabisa. Alhamdulillah, kupitia Mahfel uwezo mkubwa umefunguka. Zamani shughuli za Qur’ani zilifanyika katika makundi madogo ya kitamaduni yaliyotawanyika hapa na pale. Lakini leo, baada ya Mahfel, Qur’ani imekuwa msingi wa harakati nyingi za kitamaduni. Hili ni badiliko kubwa; hapo awali Qur’ani ilikuwa kama nyongeza katika programu nyingine, lakini sasa imekuwa kiini na msingi wake.

IQNA: Umekuwa ukisema mara nyingi kwamba Qur’ani inapaswa kuingizwa katika maisha ya kila siku na isibaki tu katika kusoma na kutarajia thawabu. Unamaanisha nini hasa?
Shakernajad: Kwa miaka mingi tumekuwa tukizungumza kuhusu Qur’ani, lakini swali la msingi ni hili: ikiwa Qur’ani hujenga mwanadamu, kwa nini athari yake haionekani wazi katika maisha yetu? Jibu lake ni rahisi — hatujajisalimisha kikamilifu kwa Qur’ani. Kwa bahati mbaya hata katika uongozi wa shughuli za kitamaduni kuna mzunguko wa maneno yanayojirudia: watu husema “tukifanya hivi basi yatatokea yale,” lakini hakuna anayechukua hatua. Maendeleo hayatokani na “lau kama”; yanatokana na mwendo na vitendo.
Qur’ani ni kitabu kinachomjenga mwanadamu, ni dawa ya kuponya nafsi, na ni mwongozo unaomuondoa mtu katika upotovu. Tukiamini kweli hayo, basi mabadiliko lazima yaanze ndani yetu wenyewe kwa kuiruhusu Qur’ani itiririke katika maamuzi yetu, mahusiano yetu, na mwenendo wetu wa kila siku.
IQNA: Baadhi ya wakosoaji wanasema kwamba hali ya furaha katika Mahfel haiendani na uzito wa mada za Qur’ani. Unasemaje kuhusu hilo?
Shakernajad: Qur’ani yenyewe imejaa furaha, matumaini na uzuri. Vipindi vya Qur’ani si lazima viwe rasmi na vizito kila wakati. Ni wajibu wetu kuwasilisha kwa watu furaha chanya na ya kiroho inayotokana na Qur’ani. Furaha hii si burudani tupu; ni matokeo ya uhai wa kiroho. Kijana anaposikiliza akiwa na tabasamu na shauku, au anaposhiriki kwa hamasa katika shughuli ya Qur’ani hilo pekee linaonesha kwamba Qur’ani imeanza kuchukua nafasi katika moyo wake.
4340842