IQNA

Chama cha Leba Uingereza katika changamoto, wagombea huru Waislamu wajipanga

17:28 - April 27, 2026
Habari ID: 3482170
IQNA – Kwa zaidi ya miaka 50, Chama cha Leba kimekuwa kikichukulia Newham, Uingereza kama ngome yake salama ya kisiasa.

Hata hivyo, tarehe 7 Mei, dhana hiyo inakabiliwa na mtihani mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa.

Wimbi la wagombea huru wanaoungwa mkono na Waislamu linaibuka kwa kasi, likilenga kugeuza hasira juu ya mauaji ya kimbari Gaza na madai ya kutelekezwa kwa masuala ya ndani kuwa athari halisi katika sanduku la kura, kwa lengo moja kuu: kuifanya Leba iwajibike kisiasa siku ya uchaguzi.

Kadri Manispaa ya Newham jijini London inavyoelekea katika uchaguzi muhimu wa serikali za mitaa na umeya tarehe 7 Mei, harakati ya kisiasa ya kimyakimya lakini yenye azma imara inaendelea kushika kasi. Muungano wa wagombea huru wanaoungwa mkono na Waislamu unatafuta si tu uwakilishi, bali pia kuwawajibisha Labour baada ya miezi ya kutoridhika miongoni mwa wananchi.

Kwa miongo kadhaa, Newham imekuwa ngome ya Labour katika Mashariki mwa London. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965, chama hicho kimekuwa kikitawala baraza la manispaa, na hata mwaka 2022 kilishinda kwa kishindo viti 64 kati ya 66. Hata hivyo, uthabiti huo sasa unaonekana kuyumba, hasa huku wakazi wengi, hususan Waislamu, wakionyesha kutoridhishwa na uongozi wa chama hicho.

Uasi Uliochochewa na Gaza

Kiini cha changamoto dhidi ya Leba ni Newham Independents Party (NIP), kundi la wagombea wengi wao wakiwa Waislamu wanaowania viti vya baraza na nafasi ya meya wa Newham.

Kikiwa kimeanzishwa mwaka 2024, kundi hilo limejipatia umaarufu kwa kampeni zake za kuunga mkono Palestina na kupinga sera za Leba, na tayari limepata mafanikio ya haraka. Kwa sasa lina viti vinne katika baraza la manispaa, na katika uchaguzi mkuu wa 2025, mgombea wao Sophia Naqvi alishika nafasi ya pili katika jimbo la West Ham na Beckton kwa kupata kura zaidi ya 7,000.

NIP ina matumaini kuwa kuongezeka kwa malalamiko ya kitaifa dhidi ya Labour, ikiwemo kashfa, msimamo wake wa sera za nje unaoonekana kuiunga mkono Israel, kushindwa kukabiliana na mrengo mkali wa kulia, pamoja na kupanda kwa gharama za maisha, kutachochea kuongezeka kwa uungwaji mkono kwao.

Mgombea wa umeya wa NIP, Mehmood Mirza, amesema: “Mashariki mwa London imechoka kupuuzwa nyumbani na kusalitiwa kimataifa. Jamii zetu zinahitaji usalama mitaani, makazi bora na haki kwa Gaza. Wagombea huru wanaibuka kwa sababu wananchi wanataka ujasiri, uadilifu na mabadiliko ya kweli.”

Wanaharakati wa ndani wanasema Labour haionyeshi tena misimamo ya kimaadili ya wakazi wa Newham, ambayo ina moja ya idadi kubwa zaidi ya Waislamu nchini Uingereza.

Mafanikio ya kundi hilo yanaashiria kuwa hii si siasa za maandamano tu, bali ni juhudi mahsusi za kujenga mbadala wa kisiasa unaojikita katika masuala ya ndani kama makazi, fedha za halmashauri na uwajibikaji, huku pia ukidhihirisha mwamko mpana wa kisiasa miongoni mwa Waislamu wa Uingereza uliochochewa na hasira kuhusu mauaji ya kimbari yanayotekeleza na utawala wa Israel huko Gaza na hitaji la uwakilishi wa kweli.

Je, Leba Inaweza Kushindwa? Licha ya changamoto hii, bado ni mapema kutabiri kuanguka kamili kwa Labour Newham. Chama hicho bado kina wingi mkubwa wa viti na miundombinu imara ya kisiasa. Hata hivyo, uchaguzi huu unaonekana kuwa tofauti sana na mingine iliyopita.

Wingi wa wagombea, mgawanyiko wa kura, na muunganiko wa malalamiko ya ndani pamoja na hasira za kimataifa umeunda mazingira yanayoweza kuleta mabadiliko makubwa. Wachambuzi wanasema hata kama Labour itahifadhi umeya, kupoteza idadi kubwa ya viti kunaweza kuwa tetemeko la kisiasa katika Mashariki mwa London.

Harakati kama hizi pia zinashuhudiwa katika maeneo mengine yaliyokuwa ngome za Labour kama Redbridge, Birmingham na Bradford, ambako wagombea huru wanaounga mkono Palestina wanaongoza mwelekeo huo.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2021, Newham ina wakazi 382,984 na ni miongoni mwa maeneo yenye mchanganyiko mkubwa wa makabila nchini. Hakuna kundi moja la kikabila lenye wingi, huku Wabangladesh wakiwa asilimia 15.9 na Waingereza weupe asilimia 14.8.

Aidha, eneo hilo lina asilimia 32 ya Waislamu, ikiwa ni ya pili kwa ukubwa nchini baada ya Tower Hamlets, na pia lina ukuaji wa kasi wa idadi ya watu, jambo linalofanya kura ya Waislamu kuwa na uzito mkubwa.

NIP italazimika kuwahamasisha Waislamu pamoja na kuvutia wapiga kura wengine wasiokuwa Waislamu, hasa wale waliokata tamaa na Labour. Hata hivyo, Chama cha Green kinaweza kuwa kikwazo, kwani nacho kinapata uungwaji mkono kutoka kwa wapiga kura wa zamani wa Labour na baadhi ya Waislamu.

Matokeo ya kura yatakapohesabiwa tarehe 7 Mei, athari zake zitasikika mbali zaidi ya Newham. Ushindi mkubwa wa wagombea huru wanaoungwa mkono na Waislamu utaashiria mabadiliko katika mwenendo wa kisiasa wa Waislamu wa Uingereza, kutoka uaminifu wa vyama vya jadi kuelekea siasa zinazozingatia misingi na masuala mahsusi.

3497248

Habari zinazohusiana
captcha